Jeraha kumweka nje kiungo Doucoure wa Everton kwa wiki 10 zijazo

Jeraha kumweka nje kiungo Doucoure wa Everton kwa wiki 10 zijazo

Na MASHIRIKA

KIUNGO mzoefu wa Everton, Abdoulaye Doucoure sasa atasalia nje kwa kipindi cha wiki 10 zijazo kuuguza jeraha la mguu.

Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 28 alikosa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Chelsea baada ya kuondolewa uwanjani wakati wa mchuano wa awali uliowakutanisha na West Bromwich Albion mnamo Machi 4, 2021.

Sogora huyo raia wa Ufaransa amepangwa kwenye kikosi cha kwanza cha Everton katika jumla ya mechi 25 zilizopita tangu aingie katika sajili rasmi ya klabu hiyo kutoka Watford mwishoni mwa msimu uliopita.

Kocha Carlo Ancelotti wa Everton amesema ni matarajio yake kwamba Doucoure atarejea kikosini kuendelea kuwatambisha kabla ya kampeni za msimu huu wa 2020-21 kutamatika rasmi.

Ancelotti pia amethibitisha kwamba kiungo James Rodriguez hatakuwa kikosini mwao hadi michuano ya kimataifa itakayosakatwa mwishoni mwa mwezi huu kukamilika.

Rodriguez amekuwa akiuguza jeraha la mguu ambalo limemweka nje ya mechi tatu zilizopita. Ancelotti amekiri kwamba azma yake ni kumruhusu nyota huyo raia wa Colombia aliyejiunga nao kutoka Real Madrid kupona kabisa kabla ya kuanza kuwajibishwa tena.

Ina maana kwamba Rodriguez, 29, atakosa mechi ijayo itakayowakutanisha Everton na Burnley ligini mnamo Machi 13 na gozi la robo-fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester City mnamo Machi 20, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Sheffield United waagana rasmi na kocha Chris Wilder

Vijana wataka wapewe nafasi katika miradi ya ujenzi wa...