Michezo

Jeraha la De Bruyne lamnyima Pep usingizi

March 5th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City amesema huenda jeraha litakalomweka nje nyota Kevin De Bruyne kwa mara nyingine likayumbisha kampeni zao.

De Bruyne ambaye ni mzawa wa Ubelgiji, alilazimika kuondoka uwanjani katika kipindi cha kwanza katika mchuano wa EPL uliowakutanisha na Bournemouth wikendi jana.

Hata hivyo, Man-City walisajili ushindi wa 1-0 katika mechi hiyo uwanjani Dean Court. Bao la mabingwa hao watetezi wa EPL lilifumwa wavuni na kiungo Riyad Mahrez kunako dakika ya 55.

“De Bruyne atasalia mkekani kwa kipindi fulani. Huenda tukio hili likatuathiri,” akasema Guardiola kwa kufichua kwamba mwanasoka huyo amekuwa akisumbuliwa mara kwa mara na jeraha la paja.

Ushindi wa Man-City ulitosha kuwarejesha kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 71 na hivyo kuendeleza presha zaidi kwa Liverpool ambao jana walikuwa na kibarua kizito dhidi ya Everton katika gozi la Merseyside.

Mbali na jeraha la De Bruyne, hofu zaidi kambini mwa Man City ilichangiwa na tukio la kuumia kwa beki John Stones mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Beki wa Manchester City, Kyle Walker (kati) amsaidia kiungo Kevin De Bruyne (kulia) kunyanyuka mara baada ya kupata jeraha City walipokabiliana na Bournemouth Machi 2, 2019, uwanjani Vitality. Picha/ AFP

“Hali kwa sasa si nzuri. Itatulazimu kujihadhari zaidi katika mechi zote zilizopo mbele yetu. Tumecheza mechi 25 chini ya siku 93. Hii ni wastani ya michuano mitatu kila wiki,” akasema Guardiola kwa kusisitiza kwamba atapania sasa kukibadilisha kikosi chake mara kwa mara ili kuweka hai matumaini ya kunyanyua mataji mengine yote ya haiba kubwa muhula huu.

Kulingana na Guardiola, majeraha yanayotishia kwa sasa kukilemaza kikosi chake ni zao la kuwachezesha baadhi ya wachezaji katika takriban kila mchuano.

“Ratiba katika kampeni za Man-City ni ngumu zaidi. Tungali katika mapambano matatu yenye ushindani mkubwa msimu huu,” akaongeza kocha huyo ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Barcelona na Bayern Munich.

Man-City waliweka hai matumaini ya kutia kapuni jumla ya mataji manne msimu huu baada ya kupepeta Chelsea 4-3 yapata majuma mawili yaliyopita katika fainali ya Carabao Cup. Kikosi hicho kinafukuzia pia ufalme wa Ligi EPL, Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Kombe la FA hadi kufikia sasa.

Chini ya Guardiola, miamba hao wa soka ya Uingereza walitawazwa wafalme wa Carabao (League Cup) baada ya kuchabanga Chelsea ugani Wembley kwa mikwaju ya penalti. Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa Man-City kutia kapuni ufalme wa League Cup kupitia penalti baada ya kuwapiku Liverpool mnamo 2016.