Michezo

Jeraha la Fernandinho latia Manchester City pabaya

February 28th, 2019 2 min read

MANCHESTER, UINGEREZA

HUENDA Manchester City ikacheza mechi tano bila uwepo wa mastaa wao, Fernandinho na Laporte Aymeric ambao waliumia Jumapili kwenye fainali ya Carabao Cup dhidi ya Chelsea.

Fernandinho ni kiungo tegemeo katika kikosi cha kocha Pep Guardiola, wakati Laporte akiwa mlinzi bora wa kikosi hicho.

Nyota hao waliumia misuli na sasa wataungana na mastaa wenzao John Stones na Gabriel Jesus ambao wanaendelea kufanya mazoezi mepesi huku wakitarajiwa kurejea watakapokabiliana na Swansea.

Baada ya mapumziko ya wiki ya mechi za kimataifa, Manchester City itaanza na Fulham hapo Machi 30.

Kabla ya mechi hiyo, City walikutana na West Ham ambapo Sergio Aguero alifunga penalti katika dakika ya 59 na kuipa City ushindi wa 1-0.

Baadaye watacheza na Bournemouth na Watford ligini, kabla ya mkondo wa pili wa mechi za Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Schalke, na baadaye robo-fainali ya FA Cup dhidi ya Swansea.

Kiungo wa Manchester City, Fernandinho (kulia) apambana na kiungo wa Chelsea N’Golo Kante kwenye fainali ya dimba la League Cup uwanjani Wembley, London. Picha/ AFP

Kuhusu nani wa kujaza nafasi ya Fernandinho, Guardiola alisema: “Danilo anaweza kucheza pale, pia kuna Ilkay Gundogan, Fabian Delph na hata Oleks Zinchenko.”

“Hali ikuwa mbaya zaidi, hata Kevin De Bruyne anaweza kujaza nafasi hiyo. Tutatafuta mbinu za kuhakikisha nafasi hiye imejazwa vyema,” aliongeza Guardiola.

“Akiwa na Santos, Dani alikuwa akicheza katika nafasi hiyo, kwa hivyo anaweza pia kuijaza vyema.”

Kocha huyo alisema amemtaka kila mchezaji ajitahidi katika mechi 11 zilizobakia ligini katika juhudi zao za kuwania ubingwa wa ligi hiyo.

“Sitaki mtu aniambie amechoka, kuniuliza ni mechi ngapi zimebakia,” Guardiola alisema Jumatano alipokuwa akiandaa vijana wake dhidi ya West Ham.

“Sharti kila mtu awe tayari kupigana hadi dakika ya mwisho, ili tuhifadhi ubingwa,” aliongeza.

“Kila mtu atahitajika kukimbia kwa kasi na kucheza kwa bidii ili tufaulu. Kwa kipindi cha miezi miwili ijayo, lazima kila mtu ajitahidi vilivyo. Tuna kikosi imara, kila mtu yuko tayari kucheza, hata wale wa akiba wako katika hali njema ya kucheza.”

“Ningependa kila mtu aonyeshe nia ya kutaka taji hili. Lazima wajitolee kwa vyovyote vile. Sijali jinsi tutakavyocheza. Nalitaka kombe lirejee kabatini. Tukishinda taji, mara moja tunaanza kujiandaa kwa lifuatalo. Nitawaangalia usoni na nitawaambia ninachotarajia baadaye,” alisema Guardiola.