Michezo

Jeraha la goti lamweka Wanyama nje tena

November 2nd, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

VICTOR Wanyama atakosa mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza klabu yake ya Tottenham Hotspur itakapokabiliana na Wolves uwanjani Molieux hapo Novemba 3 baada ya nyota huyo Mkenya kuumia goti lake tena.

Spurs imetoa taarifa kuhusu jeraha lake saa chache baada ya kusakata dakika 90 wakati timu yake ikicharaza West Ham United 3-1 Oktoba 31 na kuingia robo-fainali ya Carabao Cup.

“Victor Wanyama hatachezea Spurs wikendi hii baada ya kupata jeraha la goti Jumatano dhidi ya West Ham,” Spurs imechapisha ujumbe huo kwenye mtandao wake wa kijamii wa Twitter hapo Ijumaa jioni.

Nahodha huyu wa Harambee Stars anaungana mkekani na Mbelgiji Jan Vertonghen (jeraha la mguu), Waingereza Danny Rose (jeraha la kinena) na Eric Dier (jeraha la misuli ya paja) na Mholanzi Vincent Janssen (jeraha la kifundo).

Wanyama alijiunga na Spurs kwa kandarasi ya miaka mitano kutoka Southampton mwezi Julai mwaka 2016 kwa kiasi kinachoaminika kuwa Sh1.4 billion. Amechezea Spurs mechi 77 katika mashindano yote zikiwemo 36 msimu 2016-2017, 18 msimu 2017-2018 na tatu kwenye Ligi Kuu ya 2018-2019.

Alikuwa nje miezi minne ya kwanza ya msimu 2017-2018 akiuguza jeraha la goti alilopata dhidi ya Chelsea.

Wanyama alirejea mazoezini Desemba katikati kabla ya kusakata mechi yake ya kwanza Januari 2, 2018 akiingia mechi dhidi ya Swansea City kama mchezaji wa akiba.

Kabla ya msimu huu wa 2018-2019 kuanza, Wanyama aliumia goti tena katika mechi ya kujiandaa kwa msimu mpya dhidi ya Barcelona. Miezi miwili baadaye, Wanyama alianza mechi yake ya kwanza kwenye soka ya Carabao Cup dhidi ya Watford, ambayo Spurs ilishinda kupitia kwa penalti 4-2.

Alipata jeraha la misuli ya paja Kenya ikichuana na Ethiopia katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) hapo Oktoba 14 jijini Nairobi ambayo alifunga penalti Harambee Stars ikishinda 3-0. Jeraha hili lilimweka nje Spurs ikimenyana na West Ham kwenye Ligi Kuu hapo Oktoba 20.

Hakutumiwa katika mechi ya Klabu Bingwa Ulaya kati ya Tottenham na PSV Eindhoven iliyokamilika 2-2 mnamo Oktoba 24 nchini Uholanzi. Alirejea dhidi ya West Ham katika Carabao Cup mnamo Oktoba 31, lakini akaumia tena goti.