KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Pigo zaidi kwa Ufaransa baada ya kubainika jeraha la goti litamweka beki Lucas Hernandez nje ya mechi zote zilizosalia

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Pigo zaidi kwa Ufaransa baada ya kubainika jeraha la goti litamweka beki Lucas Hernandez nje ya mechi zote zilizosalia

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi wa Kombe la Dunia, Ufaransa, wamepata pigo jingine baada ya beki Lucas Hernandez kupata jeraha la goti ambalo sasa litamweka nje ya kampeni nzima ya kipute hicho mwaka huu.

Nyota huyo wa Bayern Munich aliye na umri wa miaka 26 aliumia goti la kulia wakati wa mechi ya Kundi D iliyoshuhudia Ufaransa wakipepeta Australia 4-1.

Kuondolewa kwa Hernandez katika kikosi cha Ufaransa kunalemaza zaidi uthabiti wa miamba hao ambao tayari wanakosa huduma za wanasoka nyota kutokana na majeraha. Hao ni Karim Benzema, N’Golo Kante, Paul Pogba, Presnel Kimpembe na Christopher Nkunku.

“Namsikitikia sana Lucas. Tumepoteza mchezaji tegemeo na mpambanaji wa kweli,” akasema kocha Didier Deschamps.

Ukubwa wa kiwango cha jeraha la Hernandez ulibainika Jumatano asubuhi baada ya sogora huyo kufanyiwa vipimo vya MRI.

Sogora huyo aliumia katika dakika ya 13 sekunde chache kabla ya Australia kufunga bao lao la pekee dhidi ya Ufaransa.

Nafasi ya Hernandez ilijazwa na kaka yake, Theo, anayesakatia AC Milan ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A). Mabao ya Ufaransa dhidi ya Australia yalifumwa wavuni kupitia kwa Adrien Rabiot, Kylian Mbappe na Olivier Giroud aliyecheka na nyavu mara mbili.

Benzema ambaye ni mshindi wa taji la Ballon d’Or mwaka huu, aliondolewa katika kikosi cha Ufaransa mnamo Novemba 20 baada ya kupata jeraha la paja akiwa mazoezini.

Nafasi yake haikujazwa na Deschamps ambaye kwa sasa ana wachezaji 24 pekee kambini baada ya Hernandez naye kuumia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Morocco watoshana nguvu na...

Wabunge wa Azimio wataka Chebukati, Guliye, Molu...

T L