Jeraha la mguu kumweka nje nahodha wa Aston Villa, Grealish, kwa mwezi mmoja ujao

Jeraha la mguu kumweka nje nahodha wa Aston Villa, Grealish, kwa mwezi mmoja ujao

Na MASHIRIKA

KOCHA Dean Smith wa Aston Villa amesema ataanzisha uchunguzi kuhusu kisa ambapo habari za jeraha la kiungo na nahodha wao, Jack Grealish, zilifichuka zaidi ya saa 24 kabla ya kupigwa kwa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowashuhudia wakitandikwa 2-1 na Leicester City mnamo Jumapili.

Grealish hakuwajibishwa katika mchuano huo kutokana na jeraha la mguu, tukio lililotamatisha rekodi yake ya kuwajibishwa na Villa kwenye mechi 48 mfululizo za EPL.

Kwa mujibu wa Smith, Grealish atakuwa mkekani kwa takriban mwezi mmoja ujao. Hata hivyo, amesisitiza kwamba kufichuka kwa habari za jeraha la sogora huyo raia wa Uingereza kulichangia zaidi motisha ya Leicester hata kabla ya kushuka uwanjani kupepetana nao.

“Nilijisomea kwenye mitandao ya kijamii kwamba Grealish asingekuwa sehemu ya kikosi cha Villa dhidi ya Leicester. Niliziona habari hizo zaidi ya saa 24 kabla ya mechi. Iwapo uchunguzi wetu utabaini kwamba aliyefichua hayo ni mtu katika kambi yetu ya mazoezi, basi tutamwadhibu vikali,” akasema Smith.

Grealish alipata jeraha hilo wakicheza dhidi ya Brighton uwanjani American Express Community mjini Brighton, Februari 13, 2021.

Villa kwa sasa wanashikilia nafasi ya nane kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 36 sawa na Tottenham Hotspur ya kocha Jose Mourinho.

Watapepetana na Leeds United mnamo Februari 27 kabla ya kuvaana na Sheffield United, Wolves, Newcastle United na Tottenham katika mechi za Machi 2021.

Grealish anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Uingereza kwenye mechi tatu zijazo za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar. Kikosi hicho cha kocha Gareth Southgate kitapepetana na San Marino (Alhamisi, Machi 25), Albania (Jumapili, Machi 28) na Poland (Jumatano, Machi 31).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Manchester City wazamisha chombo cha Arsenal na kuanza...

Messi aweka rekodi katika sare ya 1-1 kati ya Barcelona na...