Michezo

Jeraha la Ronaldo pigo kwa Juventus

March 27th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, UFARANSA

HUENDA staa Cristiano Ronaldo wa klabu ya Juventus akakosa mechi mbili muhimu kutokana na jeraha alilopata majuzi timu ya taifa lake la Ureno ikicheza na Serbia kwenye mechi ya mchujo wa Euro 2020 iliyomalizika kwa sare ya 1-1.

Matokeo hayo yalifuatia mengine ya 0-0 dhidi ya Ukraine katika mechi nyingine ya Kundi B iliyochezewa jijini Lisbon, siku ambayo Luxembourg walitoka nyuma na kuagana 2-2 na Lithuania.

Ronaldo ambaye atafanyiwa vipimo vya kimatibabu ameumia wakati klabu yake inajiandaa kukabiliana na Amsterdam Ajax katika pambano la robo-fainali ya Klabu Bingwa mnamo Aprili 10, kabla ya kurudiana jijini Turin wiki moja baadaye.

Hata hivyo, mshambuliaji yuyo huyo matata aliwaambia wanahabari: “Sibabaiki kamwe, nauelewa mwili wangu vyema. Bila shaka nitarejea kabla ya wiki mbili kuisha.”

Kwingineko, Ukraine iliinyuka Luxembourg 2-1 kutokana na bao la kujifunga la Rodrigues Gouveia, ushindi ambao umewapeleka hadi kileleni mwa kundi hili wakiwa na pointi nne, wakati Ureno wakijivunia mbili kutokana na mechi mbili.

Katika Kundi H, Uturuki iliwacharaza Moldova 4-0, mawili yakipatikana kupitia kwa Genk Tosun wa Everton, huku mengine yakifungwa na Ali Kaldirim na Kaan Ayhan.

Rais wa taifa hilo, Recep Tayyip Erdogan aliwatembelea wachezaji katika chumba cha wachezaji kubadilishia ngumu kuwapongeza kutokana na ushindi huo.

Ufaransa yashinda

Hatimaye, Uturuki walibanduliwa kutoka kileleni na Ufaransa ambao waliibuka na ushindi wa 4-0 dhidi ya Iceland kwenye mechi nyingine baadaye.

Samuel Umtiti anayechezea klabu ya FC Barcelona alitangulia kuona lango kabla ya mabao mengine kupatikana kutoka kwa Olivier Giroud, Kyalian Mbappe na Antoine Griezmann.

“Tumeshinda, lakini tulipata upinzani mkali kutoka kwa wapinzani wetu ambao walikuwa na ukuta mgumu,” alisema, Didier Deschamps, kocha wa Ufaransa.

Iceland ambao wameshinda mechi moja kufikia sasa baada ya kujibwaga uwanjani mara 17, walicheza kwa bidii lakini mbinu zao hazikuvuruga juhudi za Les Bleus.

“Tulijua haingekuwa rahisi, lakini mabao yao ya mapema yaliangamiza matumaini yetu. Mara tu walipofanikiwa kufunga bao la pili, tulichanganyikiwa kabisa, Ufaransa ni timu nzuri,” alisema kocha wao, Erik Hamren.

Albania waliichapa Andora 3-0 na kupanda hadi nafasi ya tatu, wakati Kosovo wakiagana kwa sare ya 1-1 na Bulgaria mjini Pristina.

Hapo awali, Ufaransa ilianza michuano hii kwa ushindi wa 4-1 dhidi ya Moldova, kutokana na mabao ya Antoine Griezmann, Raphael Varane, Olivier Giroud na Kylian Mbappe, wakati Viladimir Ambros akiwafungia wenyeji.

Wapinzani wa Uingereza katika Kundi A, Bulgaria na Montenegro walifungana 1-1 jijini Sofia, wakati Argentina wakinyukwa 3-1 na Venezuela jijini Madrid katika pambano la kirafiki. Staa Salomon Rondon alikuwa miongoni mwa waliofunga kwa upande wa washindi.