Michezo

Jeraha lakomesha marejeo ya Arjen Robben

September 14th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MAREJEO ya Arjen Robben katika soka yalidumu kwa dakika 28 pekee baada ya kupata jeraha katika mchuano uliokamilika kwa waajiri wake Groningen kupokezwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa PSV Eindhoven katika mchuano wa kwanza wa Ligi Kuu ya Uholanzi msimu huu.

Robben, 36, alitangaza kustaafu soka mnamo Julai 2019 baada ya kujivunia taaluma ya kuridhisha zaidi kambini mwa Bayern Munich.

Hata hivyo, alirudi ulingoni mnamo Agosti 2020 kwa kuingia katika sajili rasmi ya Groningen waliowahi kumpokeza malezi ya awali kabisa katika soka.

Katika mchuano wake wa kwanza kambini mwa Groningen tangu 2018, Robben alilakiwa na mashabiki 6,049 ila akaondolewa katika dakika ya 28 baada ya kupata jeraha.

Nyota huyo aliyewajibishwa mara 96 na timu ya taifa ya Uholanzi, alijitwalia mataji mengi ya haiba akivalia jezi za PSV, Chelsea, Real Madrid na Bayern, likiwemo kombe la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) akiwa mchezaji wa Bayern mnamo 2013.

Katika msimu wake wa mwisho kambini mwa Bayern, Robben aliwajibishwa mara 19 katika muhula wa 2018-19 na mchuano wake wa mwisho ulikuwa ushindi wa 3-0 uliosajiliwa na Bayern dhidi ya RB Leipzig.

Robben alishawishiwa na Groningen kurejea kambini mwao msimu huu baada ya kuonyeshwa mafanikio ya nguli wa vikapu Michael Jordan aliyetia kapuni mataji matatu ya NBA aliporudi ulingoni baada ya kustaafu.

TAFSIRI: CHRIS ADUNGO