Michezo

Jeraha lilivyoua makali ya Victor Wanyama

January 29th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

VICTOR Wanyama alikaribishwa ulingoni kwa kichapo baada ya klabu yake ya Tottenham Hotspur kupoteza 2-0 dhidi ya Crystal Palace katika mechi ya raundi ya 16-bora uwanjani Selhurst Park mnamo Januari 27, 2019.

Nahodha huyu wa timu ya taifa ya soka ya wanaume ya Kenya almaarufu Harambee Stars ameonekana kukosa makali yake ya awali baada ya kukosa mechi 17 akiuguza jeraha.

Kocha Mauricio Pochettino aliingiza Wanyama katika nafasi ya Eric Dier baada ya kupumzisha Muingereza huyu dakika ya 63.

Wanyama, ambaye alikuwa amechezea Spurs mara ya mwisho Novemba 10, 2018 dhidi ya Palace katika mechi ya Ligi Kuu uwanjani Selhhurst Park, amekuwa akisumbuliwa na jeraha la goti, hali ambayo imeshusha kiwango chake cha soka.

Dhidi ya Palace mnamo Januari 27, Spurs ilikubali nyavu zake kuchanwa na mshambuliaji Connor Wickham dakika ya tisa na kiungo Andros Townsend aliyepachika penalti safi dhidi ya waajiri hawa wake wa zamani dakika ya 34.

Spurs ilipata fursa ya kupunguza mwanya wa magoli dakika ya 45, lakini beki Kieran Trippier akapoteza penalti iliyopatikana baada ya Patrick van Aanholt kuchezea mchezaji wa Spurs visivyo ndani ya kisanduku.

Wanyama alikuwa injini ya Spurs katika safu ya katikati alipojiunga nayo msimu 2016-2017 kutoka Southampton, lakini majeraha yakaanza kumsumbua msimu 2017-2018 na kurejea tena kumwandama msimu huu wa 2018-2019.

Amesakata mechi nane pekee msimu huu (nne katika Ligi Kuu, mbili za League Cup, moja ya Klabu Bingwa Ulaya na moja ya Kombe la FA). Amekuwa uwanjani kwa jumla ya dakika 385 pekee msimu huu mara nyingi akitumiwa kama mchezaji wa akiba tofauti na msimu wake wa kwanza alipokuwa akianza mechi sana.

Rekodi yake ya kupata majeraha ilimfanya hivi majuzi aanze kuhusishwa na kuuzwa, huku klabu yake ya zamani Celtic nchini Scotland pamoja na AS Roma (Italia) zikisemekana zinamtaka katika kipindi hiki kifupi cha uhamisho cha Januari. Hata hivyo, wakala wake Ivan Modia Yanez alisema mapema mwezi huu kwamba hakuna uwezekano wa Wanyama kutoka Spurs katika kipindi hiki cha Januari.