Michezo

Jeraha lilimweka Martial nje, Ole Gunnar asema

January 31st, 2019 1 min read

Na CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Manchester United Ole Gunnar Solskajaer amefichua kwamba winga Anthony Martial hakujumuishwa kwenye kikosi kilichotoka sare ya 2-2 Jumanne Januari 29 dhidi ya Burnley kutokana na jeraha alilolipata akishiriki mazoezi kabla ya mechi.

Akizungunza na runinga ya MUTV kabla ya mtanange huo, Solskjaer alisema kwamba Martial huenda akarejea kikosini wikendi hii wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza(EPL) dhidi ya mabingwa wa msimu wa 2015-16 Leicester City.

“Ana jeraha dogo alilolipata akiwa mazoezini. Natumai atarejea wikendi hii lakini leo hatuwezi kumchezesha,” akasema Ole Gunnar.

Martial amekuwa na msimu wa kuridhisha tangu kocha huyo achukue usimamizi wa timu hiyo baada ya kutimuliwa kwa Jose Mourinho kama mkufunzi mkuu mwaka wa 2018 kutokana na misururu ya matokeo mabaya.

Mfaransa huyo ameanzishwa katika mechi tano za EPL na alitoka katika benchi na kufunga bao wakati wa ushindi wa 3-1 Manchester waliousajili dhidi ya mahasimu wao Arsenal kwenye kipute cha kombe la shirikisho la Uingereza(FA) Ijumaa Januari 25 ugani Emirates.

Manchester United watakabiliana na Leicester ugani King Power Jumapili Februari 3 kwenye mechi kali ya EPL wakitazamia kuendeleza rekodi yao ya kutoshindwa tangu ujio wa kocha wao.