Siasa

Jeremiah Kioni kuendelea kubeba sufuria kichwani

March 16th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

KATIBU Mkuu wa chama cha Jubilee Jeremiah Kioni, amesema hatasitisha kampeni yake ya kuweka sufuria kichwani almaarufu ‘Sufuria Movement’, akisisitiza ataiendeleza hadi pale serikali itapunguza gharama ya maisha nchini.

Kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Kameme FM, Bw Kioni alisema kuwa Wakemya wengi bado wanaendelea kuteseka licha ya ahadi za serikali kwamba itapunguza gharama ya maisha.

“Huwa ninabeba sufuria popote ninapoenda. Siko tayari kusimamisha shinikizo hizo dhidi ya serikali hadi pale gharama ya maisha itapungua. Rais William Ruto alitwambia kuwa yeye ndiye atakabiliana na gharama ya maisha. Ndiyo sababu nimeamua kumwelekeza shinikizo hizi,” akasema Bw Kioni.

Alisema kuwa yeye mwenyewe ndiye amejitwika jukumu hilo la “kuwatetea” Wakenya, wala hana uungwaji mkono wowote kutoka nje.

“Kuna watu ambao wamekuwa wakidai kwamba nimekuwa nikipokea uungwaji mkono kutoka kwa watu wenye ushawishi. Ukweli ni kuwa, hili ni jukumu ambalo mimi nimeamua kulichukua mwenyewe ili kuhakikisha nimeungana na Wakenya wale wengine kuishinikiza serikali kutimiza ahadi yake ya kupunguza gharama ya maisha,” akasema Bw Kioni, ambaye pia alihudumu kama mbunge wa Ndaragwa.

Kiongozi huyo pia alikosoa baadhi ya mapendekezo ya Ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (NADCO), akisema kuwa Jubilee itapinga vipengele vinavyopendekeza kubuniwa kwa vyeo zaidi serikalini, kwa mfano Afisi ya Kiongozi wa Mawaziri na ile ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani.

Licha ya shinikizo za kiongozi huyo kwa serikali, baadhi ya Wakenya wameanza kueleza matumaini ya hali kuimarika nchini, hasa baada ya bei za mafuta kushuka.