Michezo

Jericho All Stars pazuri kuhifadhi ubingwa

March 13th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

JERICHO All Stars ilianza kwa kishindo juhudi zake kutetea taji la Super Eight Premier League (SPS8) ilipogaragaza Melta Kabiria mabao 3-1 kwenye mechi iliyochezewa uwanjani Camp Toyoyo Jericho, Nairobi.

Nao wanasoka wa kikosi cha MASA waliomaliza nafasi ya saba msimu uliyopita walionyeshwa kivumbi kikali walipogongwa magoli 3-1 na Umeme FC ugani Umeme Ziwani, Nairobi.

Nayo Makadara Junior League SA iliyoibuka kati ya timu zilizozua upinzani mkali kwenye kipute hicho mwaka jana ilipata pigo ilipokubali kulala kwa bao 1-0 mbele ya Shauri Moyo Sportiff lililofumwa na Freddy Eninga.

Umeme FC ya kocha, Hosea Akala iliteremsha vita vya kufanya kweli ambapo Joseph Makari aliitingia mabao mawili huku sajili mpya James Tunguar akitikisa nyavu mara moja.

MASA ilikuwa imetangulia kufunga bao moja kupitia Chris Oduor lililosalia la kufuta machozi. ”Nusura tuteleze ilitulazimu tukaze buti katika kipindi cha pili baada ya wapinzani wetu kuonekana kuja kwa kasi,” Joseph Makari wa Umeme alisema.

Huku akipongeza kikosi chake kocha wa Umeme alisema ”Nimefuraishwa na ushindi huo kwa kuzingatia tulipania kutumia mechi hiyo ya kufungua dimba kupima uwezo wa sajili wapya kama wanashika kasi ya wenzio.”

Kwenye matokeo ya mechi hizo, NYSA ya kocha Fredrick ‘Oti’ Otieno ilitoka nguvu sawa bao 1-1 dhidi ya Githurai Allstars ambayo ndiyo mwanzo kushiriki ngarambe hiyo.

Nayo Kawangware United na Dagoretti Former Players kila moja ililizwa mabao 2-0 mbele ya Lebanon na Metro Sports mtawalia, TUK ilinyukwa mabao 2-1 na Rongai Allstars huku Huruma Kona ikiagana sare tasa na Mathare Flames.