Michezo

Jericho All Stars yazidi kuwika

June 11th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

JERICHO All Stars iliendelea kuimarisha kampeni zake kutetea taji la Super Eight Premier League (S8PL) kwa kurarua Huruma Kona kwa mabao 5-2 kwenye mechi iliyopigiwa Camp Toyoyo Jericho, Nairobi.

Nayo Githurai All Stars na NYSA kila moja ilijiongezea alama tatu muhimu na kuonyesha zimepania kurukia usukani wa kipute hicho.

Githurai All Stars ilibebesha Kawangware United kapu la magoli 12-0 nayo NYSA ya kocha, Fredrick ‘Oti’ Otieno iliandikisha ufanisi wa bao 1-0 mbele ya Lebanon FC.

Mchezaji wa Huruma Kona, Thomas Onah (kushoto) azuiwa na Dennis Onyango wa Jericho All Stars kwenye mechi ya S8PL ugani Camp Toyoyo Jericho Nairobi. Jericho ilishinda mabao 5-2. Picha/ John Kimwere

Jericho All Stars ambayo hutiwa makali na kocha Thomas Okongo ilihitaji kufanya kazi ya ziada dhidi ya wapinzani wao ili kuzoa alama zote muhimu.

Kati ya wachezaji matata wa Jericho All Stars, Kelvin Ndung’u alipiga hat trick huku Steve Opuku akiitingia mabao mawili.

‘Kubali yaishe’

Nayo Huruma Kona ilipata mabao hayo baada ya Yayo Wale na Thomas Onah kila mmoja kutikisa wavu mara moja.

Huruma Kona ilikubali yaishe huku ikijivunia kuzaba TUK mabao 3-2 wiki iliyopita.

”Tuliingia mzigoni kwa kusudio moja kutesa na kubeba alama zote tatu, hata hivyo nashukuru wachezaji wangu waliojibiidisha na kushinda mchezo huo licha ya kutoka chini mara mbili,” kocha wa Jericho Thomas Okongo alisema.

Akitetea kikosi chake, kocha wa Huruma Kona, Erick Onyango  alisema, “Ligi Kuu ina changamoto zake ikiwemo majeruhi yaliokosti mechi yetu baada ya baadhi yao kuvalia viatu za wenzao dimbani.”

Kwenye jedwali ya kipute hicho, Jericho All Stars ingali kileleni kwa kufikisha alama 31.

Nayo Githurai All Stars inashikilia nafasi ya pili kwa kuvuna alama 24, mbili mbele ya NYSA. Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Mathare Flames ilifungwa mabao 3-0 na Melta Kabiria, TUK ilibeba mabao 3-2 mbele ya Shauri Moyo Sportiff. Nayo MASA ilifungwa mabao 2-1 na Dagoretti Former Players, Rongai All Stars ilikomoa Makadara Junior League SA bao 1-0 huku Team Umeme ikitwaa mabao 2-0 dhidi ya Metro Sports.