Michezo

Jericho Allstars, Meltah, Githurai na Flames moto

August 19th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

WAFALME wa kipute cha Super Eight Premier League (S8PL), Jericho Allstars ilikandamiza Kawangware United kwa magoli 3-0 kwenye mechi ya kusisimua iliyovutia mashabiki wengi tu akiwamo balozi wa Marekani, Kyle McCarter iliyopigiwa BP Stadium Kawangware, Nairobi.

Jericho Allstars ilitia kapuni alama tatu na kurejea kileleni siku moja baada ya kubanduliwa na Melta Kabiria.

Jericho iliteremsha soka safi na kupata bao la kwanza dakika ya 52 kupitia juhudi zake Kelvin Ndung’u. Goli hilo lilichochea wapinzani wao na kuonekana kuzinduka huku wakishambulia ngome ya wenzao kama nyuki.

Hata hivyo, Kawangware ilikosa ujanja huku Jericho ikifaulu kufunika kimiani mabao mawili kupitia Rachael Ndukwe na Engo Bundu. ”Ushindi huo huendee mchezaji wetu aliyevunjika mguu tukiwa mazoezini,” kocha wa Jericho, Thomas Okong’o alisema.

Naye kocha wa Kawangware, Laban Mwangi alisema ”Hatuna la ziada mbali tulikubali yaishe baada ya kipindi cha kwanza kuonyesha soka safi lakini bahati haikuwa upande wetu.”

Nayo Githurai Sportiff inayokuja kwa kasi ilivuna ushindi mwepesi wa magoli 3-2 mbele ya Shauri Moyo Sportiff huku Mathare Flames ikizimwa kwa goli 1-0 na Dagoretti Former Players.

Kufuatia matokeo hayo, Jericho Allstars inaongoza kwa kuzoa pointi 39, moja mbele ya Meltah Kabiria baada ya kupiga mechi 20 kila moja. Mathare Flames inafunga tatu bora kwa kufikisha alama 35, moja mbele ya TUK iliyokomoa MASA magoli 3-2.

MATOKEO YA MECHI ZOTE

Kawangware United 0-3 Jericho Allstars

MASA 2-3 TUK

Githurai Allstars 3-2 Shauri Moyo Sportiff

Lebanon FC 0-2 Melta Kabiria

Team Umeme 1-0 Rongai Allstars

Dagoretti F.Players 1-0 Mathare Flames

Metro Sports 0-0 Mathare Flames