Michezo

Jericho Allstars pazuri kuhifadhi taji

June 19th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Jericho Allstars ipo pazuri kuhifadhi taji la Super Eight Premier League (S8PL) licha ya kuteleza na kuagana sare tasa na TUK kwenye patashika iliyopigiwa uwanja wa CAV’S Kabete.

Hata hivyo, Githurai Sportiff na Mathare Flames nazo zinaendelea kuifukuzia baada ya kutwaa mabao 2-1 na 2-0 mbele ya Dagoretti Former Players na makadara Junior League SA mtawalia.

Matumaini ya Jericho Allstars ambayo hunolewa na kocha, Thomas Okong’o kuwika kwenye mechi hiyo yaligonga mwamba baada ya kikosi hicho kukosa maarifa mbele ya wenyeji wao.

”Bila shaka kutaja kuwa vita vya mechi za mkundo wa kwanza havikuwa mteremk,” kocha wa Githurai Allstars, Fredrick Otieno alisema na kudai kuwa walijifunza mengi ikiwamo jinsi ya kushughulikia mechi za presha. Kocha huyo alisisitiza kuwa wachezaji hao pia wapo pazuri kutwaa taji hilo.

Katika msimamo wa mechi hizo, Jericho Allstars yaongoza kwa alama 32, tano mbele ya Githurai Allstars inayokuja kwa kasi ingawa ndiyo kushiriki kipute hicho. Mathare Flames imefikisha alama 26 na kutinga tatu bora. Team Umeme ya nne kwa kuzoa alama 25, mbili mbele ya Melta Kabiria.

Kwenye matokeo hayo, mabingwa wa zamani Kawangware United ilizabwa bao 1-0 na MASA, Team Umeme iliilaza Lebanon bao 1-0, NYSA iliumwa kwa bao 1-0 na Metro Sports huku Shauri Moyo Sportiff ikitwaa mabao 2-0 mbele ya Huruma Kona.