Michezo

Jericho Allstars waangushwa na Meltah Kabiria

July 15th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

KAMPENI za kufukuzia taji la Super Eight Premier League (S8PL) ziliingia mkumbo wa pili kwa kasi ambapo bingwa watetezi, Jericho Allstars ilijipata ikilambishwa sakafu na Meltah Kabiria FC.

Jericho Allstars ya kocha, Thomas Okong’o ilijikuta njiapanda ilipoachia pointi tatu muhimu kwa kubugizwa mabao 2-1.

Nayo Githurai All Stars (GAS) inayokuja kwa kasi kwenye kipute hicho iliyeyusha alama mbili muhimu ilipolazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya NYSA FC katika uwanja wa Ngong Posta, Nairobi.

NYSA ambayo hunolewa na kocha, Fredrick ‘Oti’ Otieno ilitangulia kuona lango la wapinzani wao kupitia Samuel Irungu dakika ya 22. Hata hivyo ndani ya dakika nane za mwisho vikosi hivyo vilifungana mabao matatu huku Githurai All Stars ikisawazisha kunako dakika ya 89 kupitia Patrick Lugho.

Mwanzo Githurai ilisawazisha kupitia John Mungai kunako dakika ya 82 kabla ya NYSA kujibu dakika nne baadaye bao lililofumwa na Peter Ng’ang’a.

”Licha ya kuteleza na kudondosha alama mbili muhimu bado tunapania kujizatiti zaidi ili kuwapiku wapinzani wetu,” nahodha wa GAS, Patrick Lugho alisema na kuongeza kwamba ingawa ndiyo mwanzo kushiriki ngarambe wanaamini wanatosha mboga kuvuruga wapizani wao na kutwaa ubingwa wa msimu huu.

Naye nahodha wa NYSA, Issac Wambugu alisema “Tulikuwa tumejipanga kukabili wapinzani wetu kiume maana tunawafahamu kamwe hawataki mzaha.”

Naye George Maina alitikisa wavu mara moja na kubeba bingwa wa zamani, Kawangware United kuvuna goli 1-0 dhidi ya Lebanon FC uwanjani BP Kawangware, Nairobi.

Matokeo mengine:MASA 1-1 Team Umeme, Rongai All Stars 1-2 TUK, Mathare Flames 2-1 Huruma Kona na Dagoretti Former Players 1-1 Metro Sports.