Michezo

Jericho Allstars yakosa maarifa mbele ya Dagoretti Former Players

April 29th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MABINGWA wa ngarambe ya Super Eight Premier (S8PL), Jericho Allstars ilitolewa kijasho chembamba na Dagoretti Former Players kabla ya kujipatia alama moja ilipolazimishwa kutoka sare mabao 3-3 kwenye mechi iliyopigiwa Camp Toyoyo Jericho, Nairobi.

Wachezaji wa Dagoretti Former Players walikuwa tayari kuinyima Jericho Allstars nafasi ya kupaa zaidi kwenye jedwali ya kipute hicho. Hata hivyo Jericho Allstars ilifanikiwa kuweka mwanya wa alama tano baina yake na Githurai Allstars inayofunga mbili bora kwa kufikisha alama 14 baada ya kucheza mechi nane.

Nahodha wa Jericho Allstars, Kelvin Ndungu aliiweka kifua mbele alipocheka na wavu kunako dakika ya 31. Mchezo huo uliendelea kunoga huku mabingwa watetezi wakijiongezea mabao mawili kupitia Bundu Engo na Steve Opuku na kujipatia tumaini la kuvuna alama zote muhimu.

Hata hali iligeuka ghafla na Dagoretti Former Players kuvuta kombora mbili nzito ndani ya dakika nne kupitia Oscar Maloba.

Dakika tano kabla ya kipenga cha kumaliza mchezo Dagoretti Former Players ilifanya kinyume na yaliyokuwa matarajio ya wengi pale Ibrahim Kiranga alipata nafasi kuisawazishia.

”Tulikuwa tayari kubomoa Jericho Allstars lakini vijana wangu walifanya makosa mengi tu kipindi cha kwanza,” kocha wa Dagoretti Former Players, James Ateli alisema.

Mwenzake wa Jericho Allstars, Thomas Okongo alitetea kikosi chake na kusema ”Kutovuna alama zote ni hali ya soka mambo hubadilika.”

Katika msimamo wa kipute hicho, Lebanon imetua nne bora kwa alama 13, moja mbele ya Mathare Flames awali ikifahamika kama Zamalek FC.

MATOKEO YA MECHI ZOTE WIKENDI

Jericho Allstars 3-3 Dagoretti Former Players

Makadara Junior League SA 1-1 Lebanon

Mathare Flames 1-1 Team Umeme

Melta Kabiria 4-2 Metro Sports

Rongai Allstars 3-1 NYSA

TUK 1-1 Githurai All Stars