Michezo

Jericho Allstars yateleza huku NYSA ikipiga hatua

May 28th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Jericho Allstars ilipata pigo kwenye juhudi za kutetea taji la Super Eight Premier League (S8PL) baada ya kubugizwa mabao 2-1 na NYSA kwenye mechi iliyopigiwa Posta Ngong Road, Nairobi.

Nayo Githurai Allstars iliendelea kuimarisha mbio za kufukuzia taji hilo iliporarua Melta Kabiria FC mabao 3-0 huku Team Umeme ikiliza Shauri Moyo Sportiff mabao 2-0 na kupiga hatua moja mbele.

Hatua ya NYSA ya kocha, Fredrick ‘Oti’ Otieno inaonyesha inalenga kuzinduka baada ya kuanza kampeni zake vibaya.

Ushindi wa NYSA ilipata kupitia Peter Ng’ang’a na Sam Irungu waliopiga moja safi kila mmoja na kurukia tatu bora kwa alama 18 sawa na Lebanon, Metro Sports na Team Umeme tofauti ikiwa idadi ya magoli.

”Nashukuru Mungu tayari nimeanza kuona dalili za kusonga mbele baada ya kuzamia suala la utovu wa nidhamu lililokuwa limevamia baadhi ya wachezaji wangu,” kocha wa NYSA alisema na kuongeza wamepania kuendeleza mtindo wa kugawa gozi dhidi ya wapinzani wao.

Nao Erick Warutere na James Tunguar kila mmoja alitingia Team Umeme goli moja na kuibeba kuzoa alama tatu mbele ya Shauri Moyo Sportiff.

Nayo Jericho Allstars ilipata bao la kufuta machozi kupitia kombora iliyojazwa kimiani na Caleb Olilo.

Nao wasomi wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Kenya (TUK) walijipata njia panda baada ya kuchomwa bao 1-0 na Metro Sports.

Kutokana na matokeo hayo, Jericho Allstars ingali kifua mbele kwa alama 25,nne mbele ya Githurai Allstars baada ya kusakata mechi 11 na 12 mtawalia. Githurai Sportiff ni kati ya vikosi vinavyokuja kwa kwasi kwenye ngarambe ya msimu huu hali inayoifanya kupigiwa chapuo kutwaa taji.

MATOKEO YA MECHI ZOTE

Team Umeme 2-0 Shauri Moyo Sportiff

NYSA 2-1 Jericho Allstars

Dagoretti Former Players 1-0 Rongai Allstars

Metro Sports 1-0 TUK

Lebanon 0-0 Huruma Kona FC

Kawangware United 0-1 Mathare Flames

Githurai Allstars 3-0 Melta Kabiria

MASA 1-0 Makadara Junior League SA