Michezo

Jericho wachupa kileleni Super 8

July 30th, 2018 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

Jericho All Stars wamechukua uongozi wa msimamo wa Ligi Kuu ya Super 8 PL baada ya kuandikisha ushindi wa 2-0 katika mechi iliyochezewa Camp Toyoyo, Jumapili.

Kiungo mahiri, John Owalla alifunga mabao yote dakika za 23 na 89 kwenye mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki wengi.

Licha ya kuwa na pointi sawa (37) na Makadara Junior League SA, vijana hao wa James Nandwa sasa wanaongoza jedwalini. Hii ni baada ya Makadara kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya NYSA, ugani Hamza.

Miongoni mwa timu zinazowania ubingwa wa mwaka huu, ni Jericho na Makadara pekee zilizofanikiwa kuokota pointi zote tatu mwishoni mwa wiki. Mabingwa Kawangware United waliagana bila kufungana na Metro Sports ugenini.

Uwanjani Jericho, mabao mawili katika mkipindi cha pili kutoka kwa Joespeh Makali (dakika ya 51) na  Ibrahim Ochieng (dakika ya 8) yaliiwezesha Team Umeme kupata ushindi wa 2-0 dhidi ya Kayole Asubuhi na kusonga hadi nafasi ya saba jedwalini.

MASA iliilazimisha Meltah Kabiria sare ya 2-2 katika mechi iliyochezewa BP wakati Leeds United ilipata ushindi finyu wa 1-0 dhidi ya Rongai All Stars ugani.

RYSA walipanda hadi nafasi ya 12 baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Shauri Moyo Sportif katika mechi iliyochezewa uwanja wa Githogoro mtaa wa Runda.

Matokeo ya mechi za wikendi kwa ufupi:

Makadara Junior League SA 2-1 NYSA

Jericho All Stars 2-0 Zamalek

Meltah Kabiria 2-2 MASA

RongaI All Stars 0-1 Leads United

Shauri Moyo Blue Stars 0-0 TUK

RYSA 2-1 Shauri Moyo Sportif

Kayole Asubuhi 0-2 Team Umeme