Michezo

Jericho wawazidia maarifa vijana wa Githurai Super 8

April 1st, 2019 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

Mabingwa watetezi, Jericho All Stars waliandikisha ushindi finyu wa 2-1 dhidi ya Githurai All Stars katika mechi ya Ligi Kuu ya Super 8 iliyochezewa Camp Toyoyo, Jumapili. Kevin Juma alipachika wavuni bao la ushindi dakika ya 85 mechi hiyo ikielekea kumalizika.

Uwanjani humo, Makadara Junior League SA walipoteza nafasi nyingi kabla ya kuagana 1-1 na Kawangware United.

Kevin Agoi alitangulia kuifungia Kawangware dakika ya 13 kabla ya Marvin Wachai dakika ya 32.

Ushindi wa Jericho umewapeleka hadi nafasi ya tatu jedwalini wakiwa na pointi tisa, moja nyuma ya vinara Lebanon FC walio na 10.

“Nimeridhika na jinsi tulivyocheza. Vijana walicheza kulingana na ushauri wangu. Tulikuwa 10 dhidi ya 11 lakini tutimiza lengo letu,” kocha wa Jericho, Thomas Okongo alisema.

Caleb Olilo wa Jericho All Stars (Kulia) auzuia mpira huku akikabiliwa na Wisdom Ochieng wa Githurai All Stars wakati wa mechi yao ya Super 8 iliyochezewa Camp Toyoyo, Jumapili. Jericho walishinda 2-1. Picha/ John Ashihundu

Kwa upande mwingine, ilikuwa mara ya pili kwa Githurai kupoteza mfululizo baada ya ushindi mara moja na sare moja pia, matokeo ambayo yanawaacha wakinginginia katika nafasi ya 10 baada ya kujikusanyia pointi nne pekee.

“Ilikuwa mechi ngumu lakini wapinzani wetu walaifu kutoka na ujuzi wao wa muda mrefu. Tulikuwa na nafasi nyingi lakini haikuzitumia vyema,” alisema kocha wa Githurai, Fredrick Ochieng.

Kwingine, bao la James Okello alilofunga dakika ya 68 dhidi ya Mathare Flames ugani Riruta BP liliwarejesha Lebanon uongozini.

Team Umeme walipanda hadi nafasi ya pili kufuatia ushindi wao wa 2-0 dhidi ya Huruma Kona katika mechi iliyochezewa Huruma. Giovani Moses na Makari Joe walifunga mabao hayo.

Matokeo kamili ya mechi za raundi ya nne zilizochezwa mwishoni mwa wiki

Makadara Junior League SA 1-1 Kawangware United; Mathare Flames 0-1 Lebanon FC; Jericho All Stars 2-1 Githurai All Stars; Meltah Kabiria 2-3 Dagoretti Former Player FC; TUK 0-2 NYSA; Shauri Moyo Sportiff 2-0 MASA; Huruma Kona 0-2 Team Umeme; Rongai All Stars 0-0 Metro Sports.