Habari Mseto

Jeshi jipya la nzige lavamia Wajir, Tharaka Nithi

February 2nd, 2020 1 min read

Na WAANDISHI WETU

KUNDI jipya la nzige liliwasili Kaunti ya Wajir kutoka Somalia huku maafisa wakieleza wasiwasi kuhusu udhaifu wa dawa inayotumiwa kuwaangamiza.

Nzige hao wamesababisha madhara makubwa mahala kwingi nchini.

Athari zake zimeshuhudiwa kaunti 10 zikiwemo Meru, Samburu, Laikipia, Marsabit, Garissa na Tana River.

Afisa kutoka idara ya kilimo alisema kuwa nzige wamevamia kaunti hiyo Ijumaa jioni.

Bw Hassan Gure alisema nzige waliingia katika kaunti ndogo ya Tarbaj na kusambaa hadi Kutulo, Mansa na Burmayo huku wengine wakiingia mjini Wajir.

Nzige wengine walielekea lokesheni ya Ibrahim Ure Wajir Kusini.

Bw Gure alisikitika dawa za kuwanyunyizia nzige hao zimeanza kuathiri maisha ya wakazi wanaotegemea ufugaji.

‘Dawa zinazonyunyizwa kwa njia ya ndege hazijakuwa na manufaa makubwa kwa vile nzige hawa wameendelea kuenea katika kaunti nyingine,” alisema Bw Gure.

Afisa huyo alieleza ‘Taifa Jumapili’ kwamba kaunti tatu Kaskazini mwa Kenya (Wajir, Garissa na Mandera) zinategemea ndege moja tu ya Jeshi baada ya rubani mwingine kuugua na kupelekwa hospitali.

Alisema kuna mahali ndege hiyo haihudumu kwenye mpaka wa Kenya na Somalia kwa sababu za usalama.

Bw Gure alisema zaidi ya hektari 10,000 zimeathiriwa katika muda wa siku 10 zilizopita.

Zaidi ya hektari 350,000 za malisho ya mifugo zimeathiriwa kati ya Desemba 29, 2019, na Januari 30, 2020. Shirika la chakula ulimwenguni FAO lilisema zaidi ya Sh7 bilioni zahitajika kupambana na nzige hawa ambao wameathiri watu zaidi 32 milioni.

 

Taarifa ya Alex Njeru, Bruhan Makong, na Gastone Valusi