HabariKimataifa

Jeshi la Uganda lazidi kuhangaisha Wakenya Ziwa Victoria

June 18th, 2018 1 min read

RUSHDIE OUDIA, BARACK ODUOR na ELISHA OTIENO

TAHARUKI imetanda katika visiwa vilivyo Ziwa Victoria kufuatia kukamatwa kwa wavuvi wengine 12 na maafisa wa usalama wa Uganda.

Kisa hiki ambacho kimejiri siku chache baada ya maafisa watatu wa polisi kutoka Kenya waliokamatwa na wanajeshi wa Uganda kuachiliwa huru, kimewafanya Wakenya kuishi kwa hofu ya kukamatwa.

Wanasiasa ambao wanawakilisha visiwa vilivyoathiriwa wamerejelea mjadala kuhusu umiliki wa kisiwa cha Migingo wakisema wamekuwa wakizua suala hilo lakini serikali imekataa kuchukua hatua.

Mnamo Jumamosi, maafisa wa usalama wa Uganda walinasa boti mbili, wiki moja baada ya kukamata wavuvi watano kutoka Nambo Beach, Kaunti ya Siaya. Walioshuhudia kisa cha wiki iliyopita walisema maafisa wa Uganda waliwapokonya polisi wa Kenya bunduki na simu zao kabla ya kuwapeleka Namaingo kwa mashua.

Kamanda wa polisi tawala katika Kaunti ya Siaya, Patrick Lumumba alisema ni wanajeshi wanane waliohusika ambao walifika kwa mashua ya Kenya.

Na katika kisa cha Jumamosi kilichoripotiwa katika kituo cha polisi cha Usenge na mwenyekiti wa usimamizi wa Nambo Beach, Bw Gabriel Onyango, mashua mbili za Kenya zilitwaliwa na wanajeshi wa Uganda saa kumi alasiri.

Kulingana na mkuu wa kituo cha polisi cha Usenge, Crispin Nyaga, wanajeshi hao waliwakamata wavuvi sita na kuwanyang’anya samaki wengi.

“Walichukua zaidi ya kilo 400 za samaki lakini wakawaachilia wavuvi,” alisema Bw Nyaga.

Maafisa wa kitengo cha kukabiliana na dharura cha polisi wa utawala(RDU) waliwafuata na kuokoa wavuvi hao na mashua zao.

Bw Nyagah alisema eneo hilo linahitaji doria za kila mara za maafisa wa polisi wa Kenya ili kuzuia wavuvi kukamatwa na wanajeshi wa Uganda.

Siku moja kabla ya kisa cha Jumamosi, wavuvi sita kutoka kisiwa cha Ringiti walikamatwa na kuachiliwa Jumamosi baada ya kutoa pesa.

Bi Penina Aluoch, anayemiliki moja ya boti zilizonaswa, alisema wanajeshi wa Uganda waliitisha Sh18,000 ili waachilie wavuvi na vifaa walivyonasa.