Habari Mseto

Jeshi lamulikwa kwa ununuzi wa ndege kuukuu

October 1st, 2018 1 min read

Na DAVID MWERE

KAMATI ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC), inataka Wizara ya Ulinzi kueleza ilivyotumia Sh2.9 bilioni kununua ndege kuukuu za kivita.

Kwenye ripoti yake ya 2015/16, Mkaguzi Mkuu wa serikali Edward Ouko anasema ndege hizo za kivita zilinunuliwa kutoka jeshi la angani la Jordan kwa Sh1.6 bilioni kupitia mkataba uliotiwa sahihi Aprili 2007, Zachary Mwaura alipokuwa katibu wa wizara.

La kushangaza ni kuwa ndege hizo hazijawahi kutumiwa.

Ripoti hiyo pia ilizua maswali kuhusu Sh1.3 bilioni zilizotumiwa na wizara kununua vipuri moja kwa moja.

Alipofika mbele ya kamati hiyo Ijumaa wiki jana, katibu wa wizara Torome Saitoti alishindwa kueleza kwa nini mfumo huo ulitumiwa.

Afisa mkuu wa fedha katika wizara hiyo Bw Charles Muhia alisema ununuzi huo ulizingatia mazungumzo ya Kenya na Jordan

Mwenyekiti wa PAC, Opiyo Wandayi alisema sheria ya ununuzi ya 2005 hairuhusu mazungumzo baina ya serikali mbili.