Kimataifa

Jeshi laokoa wanawake 54 na watoto 95 kutoka Boko Haram

April 10th, 2018 2 min read

Na AFP

JESHI la Nigeria limesema kwamba limewaokoa wanawake na watoto 149 ambao walikuwa wametekwa nyara na kundi la Boko Haram, Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

Msemaji wa Jeshi , Onyema Nwachuku alisema kwamba mateka walioachiliwa ni wanawake 54 na watoto 95.

“Kwa sasa, waathiriwa hao wanapokea matibabu,” akasema kwenye taarifa.

Alieleza kwa maelezo kuhusu wanakotoka yatatolewa baada ya ukaguzi huo kukamilika.

Tukio hilo linajiri baada ya wasichana zaidi ya 100 waliotekwa nyara na kundi mnamo Februari kuachiliwa, baada ya mazungumzo kati yao na serikali.

Jeshi linadaiwa kuwaokoa baada ya kuvamia kambi yake moja katika eneo la Yerimari mnamo Jumapili. Ripoti zilisema kwamba jeshi lilifaulu kuwaua wapiganaji watatu kwenye operesheni hiyo, huku likiwakamata washukiwa wengine watano wanaotuhumiwa kuwa wanachama.

Hata hivyo, haikubainika mara moja wakati na mahali ambapo waathiriwa walitekwa nyara.

Watu wengi katika eneo hilo walisema kuwa wanamgambo hao wameonekana kutolegeza kamba katika kutekeleza mashambulio yake licha ya operesheni kali dhidi yake ambazo zimekuwa zikiendeshwa na wanajeshi.

“Wanamgambo hawatishiki hata kidogo na juhudi za jeshi, kwani wameendeleza vitendo vya utekajinyara,” akasema mkazi mmoja.

Katika siku za hivi karibuni, kundi hilo limepoteza udhibiti wa maeneo mengi ambayo lilikuwa likiyashikilia.

Kundi limekuwa likiendesha mapigano hayo kwa miaka 10 iliyopita, likipigania kubuniwa kwa taifa huru la Kiislamu.

 

Vifo 20,000

Mapigano hayo yanakisiwa kupelekea vifo vya watu karibu 20,000 huku wengine 2.6 milioni wakiachwa bila makao.

Katika kipindi ambacho kimekuwa kikiendeleza juhudi za kujikomboa, kimeweza kuyavamia na kuyadhibiti maeneo muhimu kama Ziwa Chad, lililo nchini Chad.

Hata hivyo, lilipoteza udhibiti wake baada ya majeshi ya Nigeria kulivamia kwa ushirikiano na majeshi ya Chad, Cameroon na Niger.

Lakini katika juhudi za kulipiza kisasi, lilijigawanya katika vikundi vidogo vidogo, ambavyo limekuwa likitumia kuendesha mashambulio katika sehemu mbalimbali.

Baadhi ya maeneo ambayo limekuwa likiyalenga ni vijiji na soko.

Mnamo Machi, kundi liliwaua watu kumi katika mji wa Rann, wakiwemo wanajeshi wanane na wafanyakazi wawili wa mashirika ya kutoa misaada.

Mnamo Februari, majeshi ya Nigeria na Cameroon yaliwaokoa watu 1,130 ambao walikuwa wakizuiliwa na kundi hilo, baada ya kutekwa nyara katika eneo la Ziwa Chad.

Ukatili wa kundi hilo ulifikia upeo wake mnamo 2014, baada ya kuwateka nyara wasichana 276 katika shule moja katika mji wa Chibok, katika jimbo la Yobe. Ingawa baadhi ya wasichana wameachiliwa, wengine 100 wangali mikononi mwa wanamgambo hao.