Habari Mseto

Jeshi latoa ahadi ya kusajili wanawake zaidi siku zijazo

February 20th, 2018 2 min read

Zoezi la kuwasajili makurutu katika jeshi la Kenya eneo la Lamu Februari 2018. Picha/ Maktaba

Na WAIKWA MAINA na NICHOLAS KOMU

WANAWAKE zaidi watajiunga na Jeshi la Kenya (KDF) katika shughuli zijazo za kuwatafuta makurutu, amesema afisa mmoja mkuu wa jeshi.

Luteni Kanali Edward Onyango alisema kwamba maafisa wakuu katika jeshi hilo wanafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba limezingatia usawa wa kijinsia katika utaratibu wake wa uajiri.

Akizungumza Jumatatu katika uwanja wa Ol Kalou, kaunti ya Nyandarua wakati wa kusajili makurutu, Bw Onyango alisema kwamba jeshi limejitolea kuhakikisha kuwa vigezo vyote vya usawa wa kijinsia vimezingatiwa.

“Tunafanya mashauriano kuhakikisha kwamba wanawake zaidi wamejiunga na jeshi katika awamu zijazo za kutafuta makurutu. Tumejitolea kuhakikisha kwamba wao pia wamepata nafasi ya kuhudumia nchi yao.

Licha ya hayo, siwezi kutaja kwa undani wa mikakati hiyo, ila kila mmoja anapaswa kufahamu kwamba kuna mikakati inayoendelea kukabili hali hiyo,” akasema.

Kwenye zoezi hilo, changamoto kuu waliyokumbana nayo katika eneo hilo ni viwango vya chini vya elimu.

 

Elimu na umri

“Tumewakataa watu wengi kwa kukosa stakabadhi zifaazo za elimu. Pia, tumeshangazwa na idadi kubwa ya watu waliopitisha umri unaotakikana. Ilitulazimu kuwakataza kushiriki katika zoezi hilo. Hata hivyo, tumeridhishwa na idadi ambayo ilijitokeza,” akasema.

Kwa majuma kadhaa yaliyopita, kumekuwa na malalamishi kutokana na idadi kubwa ya wanawake ambao walizuiwa kushiriki katika zoezi hilo.

Baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na hali hiyo ni Samburu, Kwale na Laikipia .

Awali, msemaji wa Jeshi, Kanali David Obonyo alikuwa amesisitiza kwamba jeshi limejitolea kuhakikisha linawaajiri wanawake wa kutosha, kulingana na katiba.

 

Shujaa Kimathi

Kwingineko, familia ya aliyekuwa mpiganiaji uhuru, Dedan Kimathi imeanza upya rai za kuitaka serikali ya Uingereza kufichua alikozikwa shujaa huyo.

Huo ndio ulikuwa mwito mkuu kwenye maadhimisho ya miaka 61 tangu kukamatwa kwa shujaa huyo. Mjane wake, Bi Mukami Kimathi, hakuhudhuria hafla hiyo iliyoandaliwa uwanja wa Dedan Kimathi mjini Nyeri mnamo Jumapili kutokana na matatizo ya kiafya.

Jamaa na viongozi waliohudhuria walimtaka Malkia Elizabeth wa Uingereza kukubali rai ya kumwandalia marehemu mazishi ya kishujaa.

Waliozungumza walisema Shujaa Kimathi anafaa kupewa mazishi yanayoafiki mtu wa hadhi aliyokuwa nayo alipokamatwa na kisha kunyongwa na wakoloni.