Kimataifa

Jeshi lawaua raia 13 nje ya makao yake

June 4th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

KHARTOUM, SUDAN

WAANDAMANAJI 13 waliuawa kwa kupigwa risasi Jumatatu na wanajeshi waliokuwa wakijaribu kutawanya kundi la waandamanaji ambalo limekuwa likipiga kambi nje ya Makao Makuu ya Jeshi jijini Khartoum.

Ripoti hizo zilitokea baada ya habari kuhusu milio ya bunduki mahali ambapo waandamanaji hao wamekuwa wakishiriki maandamano.

“Waandamanaji kadhaa waliuawa kwa risasi ambazo zilipigwa kwa amri ya Baraza la Kijeshi la Upokezanaji wa Mamlaka (TMC),” ripoti za awali kutoka kwa tume ya madaktari wa Sudan ikasema katika mtandao wa Twitter.

Baadhi ya wanaharakati walinukuliwa wakisema kuwa hizo zilikuwa juhudi za kuwatawanya waandamanaji hao, huku kanda za video zilizosambazwa katika mtandao wa Twitter zikionyesha watu waliokuwa wamejeruhiwa.

Shirika la AFP liliripoti kuwa maafisa wa usalama walikuwa wamemwagwa katika mitaa ya jiji hilo kwa wingi, wengine wakitumwa mahali hasa ambapo waandamanaji walikuwa.

Kulikuwa na ripoti kadhaa za maafisa wa usalama kutumia nguvu kuwatawanya waandamanaji kutoka eneo hilo ambapo wamepiga kambi kwa wiki kadhaa sasa.

“Sasa majaribio yanafanywa kutawanya waandamanaji katika Makao Makuu ya Jeshi kwa nguvu na baraza la kijeshi,” Muungano wa Wataalamu wa Sudan (SPA) ambao umekuwa ukiongoza maandamano hayo tangu Desemba ukasema.

Mauaji ya kinyama

Muungano huo ulitaja hatua hiyo kuwa “mauaji ya kinyama” na kuwataka raia kushiriki maandamano kamili ya kutoheshimu baraza la kijeshi.

Balozi wa Uingereza Jijini Khartoum, Irfan Siddiq alisema kuwa alisikia milio ya bunduki kutoka makazi yake.

Maandamano hayo ya kuketi nje ya Makao Makuu ya Idara ya Jeshi yamekuwa yakiendelea, huku viongozi wakishiriki mazungumzo kuhusu jinsi ya kupokezana mamlaka ya Sudan na kuunda serikali mpya ya kiraia.

Jeshi liliruhusu maandamano hayo kuendelea kwa masharti kuwa yafanyiwe eneo mahususi, huku Baraza la upokezanaji mamlaka (TMC) likiendelea kuendesha nchi tangu Rais Omar el-Bashir alipong’atuliwa mamlakani Aprili.

Maafisa wa usalama wa kikosi cha RSF walisemekana kuvamia mahali walipo waandamanaji hapo jana asubuhi, milio ya bunduki ikisikika, wakati waandamanji walikuwa wakikimbia kuokoa maisha yao.

Waandalizi wa maandamano hayo waliliomba jeshi kuingilia kati na kuwalinda waandamanji kutokana na maafisa wa RFS.

Waandamanaji hao wamekuwa wakiketi hata baada ya el-Bashir kung’atuka, wakilitaka baraza la kijeshi kuachia mamlaka idara ya upokezanaji mamlaka.