Habari Mseto

Jeshi litarudisha utulivu wanafunzi warejelee masomo Muhula wa Pili Pokot Magharibi?

April 10th, 2024 2 min read

NA OSCAR KAKAI

SHULE tano ambazo zilifungwa miaka miwili iliyopita kutokana na visa vya utovu wa usalama katika maeneo ya Chesegon na Cheptulel kwenye mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet bado hazijafunguliwa.

Kati ya shule hizo katika kaunti ya Pokot Magharibi ni za msingi kama Chesegon, Cheptulel, Sapulmoi, Kissa na ya upili ya Cheptulel Boys katika kaunti ndogo ya Pokot ya kati.

Zingine ni za msingi za Lonyangalem, Ptoh, Kases, Takaywa, Lonyanyalem, Pough, Kour, Songok na Karon katika kaunti ndogo ya Pokot Kaskazini.

Vile vile, ujenzi wa chuo cha kiufundi cha Chesegon ambacho kilikuwa kinajengwa ulikwama kutokana na mashambulizi na sasa maafisa wa usalama wanaishi ndani.

Baadhi ya wanafunzi kwenye shule hizo kwenye kaunti ndogo ya Pokot ya kati hawakufanya mtihani wa darasa la nane (KCPE) na ule wa gredi ya sita (KPSEA) mwaka wa 2023 kutokana na visa vya utovu wa usalama eneo hilo.

Hii ni hata baada ya waziri wa usalama wa ndani Kithure Kindiki kupeana ahadi na maagizo mara mingi shule hizo kufunguliwa na kukarabatiwa wanafunzi wengi wamesalia nyumbani.

Lakini Jumatatu, Rais William Ruto ambaye aliongea katika eneo la Sebit, kaunti ya Pokot Magharibi kwenye uzinduzi wa kiwanda cha kilinka ya saruji alisema kuwa wanajeshi watakuwa kwenye shule hizo kwa muda wa siku mbili.

Wanakarabati shule

Uharibifu katika mojawapo ya madarasa eneo la Chesegon lililoathiriwa na uvamizi wa majangili. Picha|Maktaba

Alisema kuwa jeshi na maafisa wengine wa usalama watakarabati shule hizo kabla ya wanafunzi kufungua Muhula wa Pili.

“Tuwache uhasama kati ya jamii jirani. Wanafunzi hawawezi kukosa kusoma sababu ya wakora wachache. Muhula ujao, lazima wawe shuleni,”alisema Rais Ruto.

Mwaka jana, askari wa akiba 205 walisajiliwa baada ya kupewa mafunzo ili kuimarisha usalama katika eneo hilo. Wengine walitumwa kwenye shule.

Kwa sasa, wakazi na viongozi wamelalamikia kutuma fedha ambazo zinafaa kukarabati shule hizo ili zifunguliwe.

Uchunguzi uliofanywa kwenye shule hizo unaonyesha kuwa mali nyingi iliharibiwa na majahili, madawati yaliyoharibiwa na vitabu kutapakaa sakafuni, nyasi ndefu na miti kumea kwenye uwanja wa shule hizo na hata vichuguu vya mchwa kuonekana.

Shule zinginge ambazo ziliathirika ni shule ya upili ya wavulana ya Cheptulel na ile ya wasichana ya Cheptulel ambapo majahili wamekuwa wakitatiza wakazi kwa miezi michache iliyopita.

Wanafunzi wa shule ya upili ya wavulana Cheptulel walipewa uhamisho na kuenda kusomea eneo la Surumben, umbali wa kilomita 50.

Vijiji vya eneo hilo vimesalia mahame baada ya wakazi kuhama kutoka eneo hilo kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara.

Wakazi na wasomi wa eneo hilo ambao waliandamana wakiwa wamebeba mabango yenye maandishi ya kutaka amani Ijumaa jioni walisema kuwa masomo yaliathirika na kupelekea matokeo duni ya mtihani wa KCPE.

Mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Pithpath, Musa Kariwoi alisema kuwa hali ya wanafunzi wengi wa eneo hilo haijulikani na idadi ya wanafunzi na walimu katika eneo hilo imepungua pakubwa.

Kuzipokonya silaha

Alimtaka Rais Ruto kuunganisha jamii hizo mbili na kuzipokonya silaha haramu.

Mkazi, Hellen Nichola alisema kuwa utovu wa usalama umeathiri elimu sababu wao wanaishi umbali wa kilomita tano suala ambalo huchangia wanafunzi wengi kutofika shuleni.

George Charita alisema kuwa wazazi wa eneo hilo hawana fedha za kuelimisha wanao na huwafanya wao kuwacha shule.

Paul Lomuria, mkazi alisema kuwa watoto wengi wa eneo hilo walisalia kuwa mayatima baada ya wazazi wao kuuawa.

Seneta wa Pokot Magharibi Julius Murgor aliwataka wakazi kupeleka wanao shuleni.

“Tunafaa kuishi kwa amani na majirani zetu,” alisema.

Gavana wa kaunti ya Pokot Magharibi Simon Kachapin alitaka kuwe na amani ili elimu iimarike na wanafunzi kusalia shuleni.

“Tunashirikiana na serikali kuu kuhakikisha kuwa shule hizo zinafunguliwa,” alisema.

Zaidi ya shule 50 zimeathiriwa na visa vya ujangili eneo la Kaskazini mwa Bonde la ufa.

Shule hizo ziko katika kaunti za Pokot Magharibi, Turkana, Baringo, Elgeyo Marakwet, Samburu na Laikipia.