Makala

Jezi za Kenya za michezo ya Olimpiki kuzinduliwa Aprili

March 4th, 2024 2 min read

NA TOTO AREGE
JEZI za timu ya taifa ya Kenya za Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024, zinatarajiwa kuzinduliwa sokoni mwezi ujao, Aprili, kama ilivyotangazwa na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki ya Kitaifa ya Kenya (NOC-K), Francis Mutuku siku ya Jumamosi.

Mutuku alizungumza katika semina ya wanahabari ya siku tatu iliyoandaliwa na NOC-K katika Hoteli ya Nokras Riverine na Spa huko Sagana, Kaunti ya Murang’a ambapo Rais wa NOC-K Paul Tergat alikuwepo.

“Uamuzi wa kuwasilisha bidhaa hizi uliongozwa na mahitaji kutoka kwa umma wa Kenya na soko la kimataifa kwa bidhaa zinazohusiana na Timu ya Kenya, kufuatia umaarufu wa mashati bandia yanayouzwa kimataifa,” alisema Mutuku.
Kando na jezi, vitu kama vile fulana, nguo za mazoezi, mashati ya polo, kofia, na chupa za maji, zilizoundwa ili kuendana na na rangi za taifa.
Juhudi hizi zitafanywa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hizo katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na maduka ya kijumla (Supermarkets), maduka ya michezo, maduka na vituo vya biashara rejareja.
“Tunalenga kuzindua jezi tofauti zinazolingana na matukio mbalimbali ya michezo kama vile Olimpiki, Michezo ya Jumuiya ya Madola, na Michezo ya Ufukweni. Mradi huu unalenga kuletea nchi yetu fahari ya kitaifa na umoja miongoni mwa Wakenya,” alisema Mutuku.
Ili kudumisha uhalisia na kukataza bidhaa bandia, hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watu watakaokuwa wanauza bidhaa bandia sokoni.
Mutuku aliendelea kusema kwamba; “Fedha zitakazopatikana kutoka kwa bidhaa hizo zitaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ya vijana, ikilingana na kaulimbiu ya ‘Timu ya Kenya kuhamasisha Taifa’.

Kwa kuvaa jezi hizi ambazo ni za taifa, watu wanaweza kuhisi uhusiano moja kwa moja na wanariadha wanaowakilisha nchi, kukuza hisia ya fahari na uungaji mkono.”
Bw Tergat katika hotuba yake alitaja kwamba, Kenya imekuwa ikijulikana kama Nyumbani kwa Mabingwa, kutokana na wanariadha kuleta medali nyumbani.
“Mafanikio haya yameimarisha nafasi ya Kenya kama nchi yenye mafanikio zaidi barani Afrika katika Michezo ya Olimpiki. Mafanikio ya kipekee ya wanariadha wa Kenya, hasa katika Michezo ya Olimpiki, sio tu yameinua sifa ya nchi kimataifa lakini pia yamefungua milango katika maeneo mbalimbali ya maisha yao,” alisema Tergat.

Pia, alitambua jukumu la waandishi wa habari wa michezo katika kuchapisha habari za wanamichezo wa Wakenya.

“Kama mwanariadha wa zamani, naelewa vizuri jukumu lenu la kuwahadithia mashabiki wetu na wananchi wenzetu habari zetu na majukumu makubwa mwaka huu wa Olimpiki,” aliongezea Tergat.