Habari Mseto

Jiandaeni kwa ukaguzi wa mipaka – Chebukati

February 15th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) sasa imetengaza kuwa iko tayari kuanza kubadili mipaka ya maeneobunge kuanzia Machi 2020, Hazina ya Kitaifa itakapotoa fedha na matokeo ya sensa.

Kisheria, IEBC inahitajika kuwa imekamilisha shughuli hiyo kote nchini kufikia Julai 2021, miezi 12 kabla ya Wakenya kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

Kwenye taarifa kwa vyumba vya habari Ijumaa, mwenyekiti wa tume hiyo, Bw Wafula Chebukati alisema kuwa mipaka ya sasa ya maeneo-bunge na wadi iliwekwa mnamo Machi 7, 2012 na inapaswa kufanyiwa mabadiliko kuanzia mwezi ujao.

Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa kipengele cha 89 cha Katiba ya sasa, mipaka ya maeneobunge inapaswa kubadilishwa baada ya miaka minane.

“IEBC itabadili majina na mipaka ya maeneo-bunge baada ya kipindi kisichopungua miaka minane na kisichozidi miaka 12. Lakini shughuli yoyote ya mabadiliko ya mipaka sharti ikamilike miezi 12 kabla ya uchaguzi wa wabunge,” kipengele hicho kinasema.

Lakini ibara ya kwanza ya kipengee hicho inasema idadi ya maeneobunge haiwezi kuzidi 290. Hii ina maana kuwa IEBC inaweza kupunguza idadi hiyo lakini haiwezi kuongeza idadi hiyo.

“Mipango imewekwa kuhakikisha kuwa shughuli hiyo inaendeshwa inavyapaswa, fedha zitakapotolewa na tutakapopokea data ya sensa iliyofanywa Agosti 2019 kutoka kwa Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS),” akasema Bw Chebukati.

“Kama sehemu ya matayarisho kwa shughuli hii muhimu, IEBC imeanzisha mpango wa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake, kununua vifaa hitajika kwa ajili ya kuendesha majaribio ya shughuli hiyo,” akaongeza.

Tangazo la Bw Chebukati huenda likaibua tumbojoto miongoni mwa baadhi ya wanasiasa ambao wanawakilisha maeneo yenye idadi ndogo ya watu wakihofia kuwa huenda “wakapoteza kazi” endapo maeneobunge hayo yataunganishwa na mengine.

Kwa mfano, mwaka 2019 Mbunge wa Marakwet Mashariki, Bw David Kangogo Bowen na mwenzake wa Marakwet Mashariki William Kisang walikosoa matokeo ya sensa yaliyoonyesha maeneo-bunge hayo kuwa na chini ya watu 10,000 kila moja.

“Hatukubaliani na matokeo haya kwa sababu idadi kubwa ya watu wetu hawakuwa nyumbani usiku wa Agosti 24 na 25 kwani walitorokea mijini kutokana na utovu wa usalama,” akasema Bw Bowen.