Habari Mseto

Jicho Pevu apendekeza walanguzi wa dawa za kulevya wanyongwe

March 8th, 2024 1 min read

NA WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Nyali Mohamed Ali amependekeza kunyongwa kwa walanguzi wa dawa za kulevya ambao wanaendelea kuhangaisha watoto wa Mombasa.

Hata hivyo, Bw Ali alihakikishia wakazi kuwa serikali itamaliza changamoto ya dawa za kulevya na ulanguzi eneo la Mombasa.
Bw Ali alisema licha ya viongozi wa Mombaasa kususia mkutano wa kujadili changamoto hiyo, serikali imeahidi kukomesha jinamizi hilo.

“Viongozi wa Pwani Magavana, Wabunge, Wawakilishi wa Wanawake na Maseneta walikuja mkutanoni. Lakini hapa Mombasa ni viongozi wachache tu ambao walihudhuria wengine walisusia,” alisema Bw Ali huko Likoni.

Mbunge huyo alisema viongozi wengi wa Mombasa walisusia mkutano huo ilhali Naibu wa Rais Rigathi Gachagua alinuia kujadiliana nao namna watakavyoshirikiana kukomesha janga hilo.

“Ni lazima tupige vita mihadarati, ni lazima tupambane na walanguzi wote. Kule bara, viongozi wa eneo la Mlima Kenya walimuita Rais William Ruto na Naibu wake Bw Rigathi kujadili changamoto ya pombe,” alisema.

Bw Ali alisema baada ya mkutano wa kujadili changamoto ya pombe haramu, viongozi wa Mlima Kenya walishirikiana na kuingia vichochoroni kumwaga pombe hizo.

Alisema Gavana wa Kirinyaga Bi Anne Waiguru akaamua kufunga baa zote kaunti hiyo ili alinde maisha ya wakazi hao.

Hata hivyo alisema, baada ya Bw Rigathi kuondoka viongozi wa Mombasa wakaanza kuungana na kusema hawawezi kusomea.

“Wakasema serikali inajua mahali mihadarati imo wakatafutwe. Badala ya kuunga na kutafuta mawazo ya kupambana na walanguzi mnatukana Naibu Rais. Hizi dawa za kulevya tutamaliza. Namuomba walanguzi wauawe bila huruma,” alisema.

Bw Ali ambaye ndiye mbunge pekee aliyechaguliwa kupitia chama cha UDA katika Kaunti ya Mombasa, aliwashtumu baadhi ya viongozi wa Mombasa wakiongozwa na Gavana Abdulswamad Nassir kwa kuikosoa sana serikali ya Kenya Kwanza.