Michezo

Jimenez aweka rekodi mpya Wolves

June 20th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSHAMBULIAJI Raul Jimenez aliweka rekodi ya kuwa mfungaji wa mabao mengi zaidi kambini mwa Wolves katika msimu mmoja wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kucheka na nyavu na kusaidia waajiri wake kuwapiga West Ham United 2-0 uwanjani London.

Ushindi wa Wolves uliweka hai matumaini yao ya kunogesha soka ya bara Ulaya msimu ujao. Kufikia sasa, Wolves wanashikilia nafasi ya sita jedwalini kwa alama 46 sawa na Manchester United ambao pia wanawania fursa ya kuwapiku Chelsea kwenye nafasi ya nne na kufuzu kwa kivumbi cha UEFA muhula ujao.

Jimenez ambaye ni mzawa wa Mexico alimzidi maarifa kipa Lukasz Fabianski baada ya kupokezwa krosi na mchezaji Adama Traore aliyetokea benchi katika kipindi cha pili. Bao la Jimenez lilikuwa lake la 14 katika kampeni za EPL msimu huu wa 2019-20.

Traore alichangia pia bao la pili la Wolves lililojazwa kimiani na mshambuliaji Pedro Neto aliyetokea benchi na kushirikiana vilivyo na Matt Doherty.

Matokeo ya West Ham yanawaning’iniza padogo mkiani mwa jedwali la EPL kwa alama 27, sita zaidi kuliko Norwich City wanaokokota nanga mkiani. Jaribio la kwanza la West Ham langoni pa Wolves lilitokea katika dakika ya 49 wakati ambapo tineja Jeremy Ngakia, 19, alielekeza kombora langoni pa kipa Rui Patricio.

Kampeni za Wolves msimu huu zilianza takriban siku 330 zilizopita kwa mechi ya kufuzu kwa kipute cha Europa League dhidi ya Crusaders mnamo Julai 25. Tofauti na wapinzani wao ambao wamecheza mechi chache, mchuano dhidi ya West Ham ulikuwa wa 49 kwa Wolves kupiga hadi sasa msimu huu.

Wolves kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Bournemouth uwanjani Molineux mnamo Jumatano ya Juni 24 siku moja baada ya West Ham kushuka dimbani kuvaana na Tottenham katika gozi la London.