Makala

Jimmy Gait afichua sababu za kuwa singo akiwa na miaka 44  

February 25th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MWIMBAJI wa nyimbo za injili James Ngaita Ngigi almaarufu Jimmy Gait amefichua sababu za kusalia singo, licha ya kuwa msanii tajika na mwenye hela.  

Jimmy Gait, kwenye mahojiano na mwanahabari Lynn Ngugi kupitia chaneli yake ya You-Tube, pia amesema hajui atakapooa huku umri wake ukizidi kusonga.

Mjasirimaali huyo aliambia Bi Lynn kwamba amesalia kapera kwa sababu za kukosa “bahati ya mapenzi”.

“Mimi siko kwenye ndoa,” alisema mwimbaji huyo wa kibao tajika cha ‘Huratiti’.

“Sijaoa na sijui iwapo nitafanya hivyo hata ingawa umri wangu unasonga. Wee, nimepigwa Character development,” alisisitiza Jimmy Gait.

Character development, ni kauli ya kisasa inayoashiria mtu kuhangaishwa kimapenzi kama vile kuachwa.

Akitetea sababu ya kukosa kuoa, mwanamuziki huyo aliyevuma 2013, alisema amepitia mengi mikononi mwa wanawake hivyo basi kukosa hamu ya kuoa.

“Labda sijabahatika sana katika fani hii. Wahusika ni wapande zote mbili, mimi sasa sijui. Sijui niwe kama Solomon ama?” Jimmy Gait alihoji.

Aliongeza kuwa anajitahidi huku akikiri iwapo atapata mchumba atakayemfaa, hatakuwa na budi ila kufunga ndoa naye.

Hata hivyo Jimmy Gait, 44, alitaja sifa za mwanamke anayetamani kuwa naye.

“Mimi kwangu ni utangamano. Hakika mwanamke mwerevu anayenivutia kwa urembo wa mwili lakini awe na moyo wa kujali, kuelewa basi sitafikiria mara mbili,” alielezea.

Mwimbaji huyo alilamikia tabia chwara kutoka kwa wanawake warembo, aliodai hawawapi wanaume zao amani nyumbani.

“Mwanamume anataka amani nyumbani, lakini wengi wa warembo hawakupi amani. Sisemi ni wote na sitaki kunukuliwa vibaya, lakini baadhi ya warembo hawa ni wazuri sana. Ndio, lakini wakiingia kwa nyumba…” Alieleza Jimmy Gait.

Aidha, alielezea hofu yake kuwa kwenye ndoa na mwanamke mrembo.

“Unapata huyo mwanamke mrembo hajui kupika, anakupikia ‘mashakura’, hakupi amani, anakupigia kelele, hataki kujua iwapo una pesa, bajeti kubwa. Kuelewa hali ya kifedha ya mwanaume wake, hatambui hilo,” alisema Jimmy Gait.