Habari Mseto

Jimnah Mbaru apokea Sh900 milioni, mauzo ya hisa zake Britam

April 24th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Mfanyibiashara maarufu Jimnah Mbaru alipokea zaidi ya Sh900 milioni baada ya kuuza hisa zake milioni 50 katika kampuni ya bima ya Britam.

Bw Mbaru aliuzia hisa hizo kampuni ya Switzerland, Swiss Re, iliyo na makao yake Zurich kulingana na taarifa za watu wanaolewa mkataba huo.

Haijulikani kwa yakini kiwango cha pesa alichouza hisa hizo, lakini kulingana na mdokezi, mfanyibiashara huyo alipokea pesa nyingi baada ya mauzo hayo.

“Bw Mbaru aliuza hisa kwa zaidi ya Sh17 kila moja,” alisema mdokezi huyo ambaye hakutaka jina lake kuchapishwa.

Kampuni ya Swiss Re ilifanyika ya kuwa mshikadau wa Britam mwaka jana baada ya kupata hisa 348.5 milioni kutoka kwa mfanyibiashara Peter Munga.

Mauzo hayo yameibua mjadala kuhusu uwazi miongoni mwa kampuni zilizoorodheshwa katika soko la hisa la Nairobi (NSE) na wajibu wa Mamlaka ya Masoko ya Mtaji (CMA) na sheria zilizopo kuhusu uwazi.

CMA huwa haitoi agizo kwa kampuni zilizoorodheshwa kutangaza bei ya kuuza au kununua hisa kinyume na mamlaka zingine kwingineko ulimwenguni.

Hatua hiyo, kulingana na wachanganuzi, sio nzuri kwani huwa inazuia wawekezaji wadogo walio na azma ya kununua hisa.

Kabla ya mauzo hayo, Bw Mbaru anasemekana kununua hisa 30 milioni katika soko wazi kwa bei chini ya bei aliyouzia kampuni hiyo ya Switzerland.