Habari Mseto

Jina jipya la kampuni ya Kenya Power

October 2nd, 2019 1 min read

Na MARY WANGARI

NI rasmi sasa! Kampuni ya umma ya Kenya Power and Lighting Company Limited ina jina jipya.

Hii ni baada ya shirika hilo ambalo lina wajibu wa kusambaza umeme nchini kutangaza rasmi hatua ya kubadilisha jina lake ambapo itakuwa sasa ikiitwa The Kenya Power and Lighting Company Plc.

Umma ulifahamishwa kuhusu mabadiliko hayo mapya kupitia tangazo lililochapishwa na kampuni hiyo kwenye gazeti la Daily Nation, Jumatano, Oktoba 2.

“Notisi imetolewa hapa kuwa shirika la Kenya Power and Lighting Company Limited limebadilisha jina lake ambapo litakuwa likiitwa The Kenya Power and Lighting Company Plc,” limesema tangazo hilo.

Aidha, kupitia tangazo hilo, kampuni imeeleza kuwa hatua hiyo iliafikiwa kufuatia uidhinishaji kutoka kwa Msajili wa Kampuni na maafikiano baina ya wenye hisa.

“Ni kufuatia kuidhinishwa jinsi inavyostahili na wenye hisa na baada ya kupokea cheti cha kubadilisha jina kilichotolewa na Msajili wa Kampuni,” imesema.

Kampuni hiyo ya kusambaza umeme ndiyo ya hivi punde zaidi kutii Sheria ya 2015 kuhusu Kampuni.

Mnamo Frebruari 2018 kampuni ya huduma za mawasiliano ya Safaricom vilevile ilichapisha notisi rasmi kwa umma ikitangaza kubadilisha jina lake kutoka Safaricom Limited hadi Safaricom Public Limited Company (PLC).

Kulingana na sheria hiyo, kampuni ya umma yenye idadi maalum ya hisa zinazohitajika inaweza ikasajilishwa kwa jina linaloishia kwa maneno “kampuni ya umma yenye idadi ndogo ya hisa”.

Kwa upande mwingine, kampuni ambayo ni ya binafsi na yenye idadi ndogo ya hisa inaweza kusajilishwa kwa jina linaloishia “limited” (Ltd).