Habari MsetoSiasa

Jina langu liondolewe kwa ripoti ya PAC – Monica Juma

March 21st, 2019 2 min read

NA CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Mashauri ya Kigeni Monica Juma sasa anaitaka bunge la kitaifa kumwondolea lawama kutokana na sakata ya utoaji zabuni ya bima ya Sh3.5 bilioni kwa polisi na maafisa wa magereza mnamo 2014.

Akiongea alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC) Jumanne waziri huyo alisema hakuwa afisa mwajibikaji (Katibu wa Wizara) katika Wizara ya Masuala ya Ndani wakati zabuni hiyo ilitolewa.

Mkaguzi Mkuu wa Matumizi ya Fedha za Serikali Edward Ouko kwenye ripoti yake ya mwaka wa kifedha wa 2014/2015 alisema kuwa zabuni hiyo iliyotiwa saini mnamo Julai 14, 2014 ilitolewa kinyume cha sheria.

Kandarasi hiyo ambayo ilidumu kwa miaka miwili kuanzia mwaka wa 2014 hadi 2016 ilipewa kampuni ya bima ya Pioneer Assurance ambayo ilitisha malipo ya Sh1.7 bilioni ilhali kampuni ya bima ya Britam ilitisha malipo ya Sh629 milioni. Ajabu ni kwamba kampuni ya Pioneer Assurance ndio ilipewa zabuni ya kutoa bima kwa polisi ya thamani ya Sh8 milioni kwa maafisa wa ngazi ya chini hadi Sh200 milioni kwa maafisa wa vyeo vya juu.

Kulingana na sheria ya ununuzi wa bidhaa na huduma za umma, kampuni iliyolipisha ada ya chini na kudhihirisha uwezo wa kutoa bidhaa au huduma husika ndio inapaswa kupewa kandarasi.

Jumanne Dkt Juma alisema ni aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Masuala Mutea Iringo ambaye angeweza kujibu maswali yaliyoibuliwa kwenye ripoti ya Bw Ouko na wanachama wa PAC wakiongozwa na Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi.

Maswali kuhusu utoaji zabuni kinyume sheria yamekuwa yakiibuliwa katika ripoti za Bw Ouko tangu mwaka wa kifedha za 2014/2015.

Katika ripoti yake iliyowasilishwa bungeni Novemba mwaka jana, PAC inapendekeza kuwa Dkt Juma alaumiwe kwa sakata hiyo kwa kuendelea kutekeleza zabuni hiyo alipochukua usukani kama Katibu wa Wizara hiyo baada ya Bw Iringo kuondoka.

“Natambua kuwa kandarasi hii ilitolewa kinyume cha sheria. Lakini pendekezo la kamati hii kwamba mimi ndiye nilaumiwe sio sahihi,” Dkt Juma akasema alipoulizwa na wanachama wa PAC kuhusu ni kwa nini hakusitisha kandarasi hiyo baada ya Bw Iringo kuondoka mnamo Agosti 20, 2014. Hii ni licha ya kufahamu kuwa Dkt Ouko alikuwa ameibua maswali kuhusu uhalali wa kandarasi hiyo.

Lakini Bw Iringo alipofika mbela ya kamati hiyo baadaye Jumanne alitetea kandari hiyo akisema ilizingatia mahitaji yote ya Sheria ya Ununuzi wa Bidhaa na Huduma za Umma.