Makala

Jinsi ala hii 'Wandindi' imembadilishia kijana maisha

April 5th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

NYERI ni mji wenye shughuli mbalimbali, hasa za kibiashara.

Mashambani kwa kawaida panastawi mimea mbalimbali kutegemea na msimu.

Katika kitovu cha mji wenyewe tunakutana na John Kibe ambaye jina lililopata umaarufu ni ‘Wandindi Kibe’.

Kijana huyu ni mmoja wa machale (comedians) na katika Churchil Show, kipindi maarufu katika runinga ya NTV.

Kwa hakika yeye hutumia ala hii ya wandindi kuigiza.

Wandindi ni ala ya kiasili, ambayo inaonekana kusahaulika katika kundi la ala za kucheza, lakini kwake Kibe hana nia nyingine isipokuwa kuidumisha ala hii.

Bw John Kibe, maarufu kama Wandindi Kibe, mwigizaji na chale anayetumia ala hii ya ‘wandindi’. Picha/ Sammy Waweru

Ni kifaa maalumu kinachoibua ucheshi kwa jinsi anavyokielekeza kikawa hasa kinajibu maswali kwa mujibu wa kinavyoelekezwa.

“Wandindi ndiyo kitega riziki changu, kimeniimarisha kwa kuwa nimeigiza hata mbele ya Rais Uhuru Kenyatta,” anafichua Bw Kibe.

Umbo lake ni mithili ya gitaa, kimeundwa kwa goma iliyoambwa na ngozi, na kipande cha mti. Kina waya moja inayotoa sauti, iguswapo.

Sanaa

Kibe anasema safari hii ya sanaa ilianza tangu akiwa mdogo, shule ya msingi.

Mama yake alikuwa mhudumu katika kituo cha kunusuru watoto waliotupwa, kilichoko eneo la Othaya, ambapo baadhi ya watoto walifunzwa kuunda zana za muziki.

“Kulikuwa na miradi mbalimbali, ufugaji wa sungura ukiwamo, na ngozi zao ndizo zilitumiwa kuunda wandindi. Nilijua kuitengezea huko,” anasimulia.

Alipojiunga na shule ya upili 1997, alibeba wandindi ambapo alikuwa akitumbuiza katika hafla tofauti kama vile mashindano ya nyimbo na michezo ya kuigiza.

“Nakumbuka nilipangwa katika daraja la 931J kutoa sauti ya Solo kwa kutumia zana hii. Kwenye tamasha, nikijitambulisha kwa usaidizi wa wandindi, watazamaji walifurahia kwa sababu ilizua ucheshi,” aelezea.

Ilichukua muda wa dakika nne kuigiza kwa kifaa hiki, huku mashabiki wakionekana kufurahia mwigo wa kitambulisho.

Mwaka wa 2001, baada ya kukamilisha mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne, KCSE mwaka uliotangulia, kijana huyu alijishughulisha kucheza wandindi katika hafla mbalimbali kama vile harusi na hata kanisani bila malipo.

Anaelezea kwamba alichukua mkondo huo ili kutafuta msingi wa kuimarisha talanta yake na kuijuza kwa umma.

“Harusi nilizoigiza, mashabiki walifurahia na kunipa motisha ambapo baadhi yao waliniunganisha na tamasha mbalimbali za mashindano katika kiwango cha kaunti na hata kitaifa,” adokeza.

Kukutana na Rais Kenyatta

Bidii yake ilizaa matunda kwani mwaka 2015 alishinda tuzo ya Sh100, 000 pesa taslimu katika mojawapo ya mashindano aliyoshiriki.

Pia ameshiriki katika mashindano ya kila mwaka ya MCSK Gala Awards na Dealer Of the Year Award (DOYA).

Isitoshe, chini ya utawala wa Rais Kenyatta amewahi kuigiza katika hafla ya kuadhimisha Jamhuri Dei uwanjani Nyayo, Nairobi.

“Nimetumbuiza katika harusi za baadhi ya watu mashuhuri nchini na misafara inayoandaliwa na vyombo vya habari, NTV ikiwamo,” anasema.

Ada ya chini anayotoza kwa hafla moja ni Sh10,000 akieleza kuwa malipo hutegemea na hadhi ya tamasha.

“Kuna ninazotoza hadi Sh200, 000. Kwa mwezi hupata zaidi ya hafla mbili,” aeleza, akiongeza kwamba pia hutoa mafunzo kwa wanafunzi.

Huunda wandindi na hugharimu kati ya Sh3,500 hadi Sh5,000. Ya kurembesha maskani ni kati ya Sh1, 000-2, 000. Mbali na kuigiza wandindi, Kibe pia huuza na kupiga chapa kanda za filamu na muziki, kazi anayosema aliifungua kupitia sanaa.

Je, walifahamu jina la ala hii kwa lugha mbalimbali za Kiafrika; hasa za nchini Kenya? Tutajie hapa.