Makala

Jinsi baadhi ya Wakenya huporwa mabilioni chambo kikiwa 'ahadi ya utajiri wa kuzalisha pesa'

May 10th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

AGOSTI 17, 2018, mhudumu wa bodaboda katika Kaunti ya Murang’a, Peter Njogu, alipatana na mwalimu wake wa zamani aliyemwahidi kumuonyesha njia ya kuzalisha pesa awe na ukwasi wa kasi.

Bw Peter Njogu, 34, akihudumu katika mji wa Murang’a kwa bodaboda aliyopata katika mkataba wa ‘kupunjwa akiba’. Picha/ Mwangi Muiruri

Uhusiano wao uliofuatia sasa ukiweka taswira wazi kuwa sio tu wawekezaji wa kampuni za Kasisi Peter Ngari ambazo ni Gakuyo na Ekeza ambao waliripotiwa kupoteza Sh2.4 bilioni; kuwa waliopoteza pesa zao katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni wengi.

“Mbinu ilikuwa rahisi: Nitafute Sh10,000, nihifadhi katika kundi la akiba na mikopo na moja kwa moja nihitimu kupewa pikipiki mpya ya thamani ya Sh110,000.” Afichua Bw Njogu mwenye umri wa miaka 34.

Hata hivyo, aliagizwa kuwa ni lazima angesajili marafiki zake 20 na wahifadhi Sh10,000 kila mmoja ndipo akabidhiwe hiyo pikipiki mpya.

“Nilijizatiti na nikasajili marafiki 40 ambao wengi ni wahudumu wenzangu katika sekta hii ya bodaboda. Wote walihifadhi Sh400,000 na ukiongeza zangu Sh10,000 utapata kuwa tulikuwa tumeweka kama akiba Sh410,000,” afafanua.

Anasema kuwa alikabidhiwa pikipiki mpya kama alivyoahidiwa, lakini marafiki wake wote hawakunufaika kwa kuwa kampuni hiyo ya akiba na mikopo ilijiondoa mashinani baada ya kupuja wengi pesa zao kwa njia hiyo.

Leo hii, anasema kuwa aligundua wengi walitumika kuwavutia wenzao wakatapeliwe pesa zao ndani ya mpangilio huo na kama tuzo ya kazi kuntu ya kuwaleta wengi wanyolewe bila maji kihela, wakahongwa kwa kupewa pikipiki mpya.

Ni suala ambalo limeshika kasi mashinani hapa nchini na ambapo Wakenya wasio na habari wananyonywa utajiri wao kwa njia hii ya kuahidiwa utajiri wa haraka.

Gavana wa Murang’a, Mwangi Wa Iria anasema: “Ndio, kuna haya makundi ambayo yametua mashinani na ambayo yanajisajili kama kampuni za akiba na mikopo na kumeanza kuchipuka vilio hapa na pale kuwa wengi wamezamisha utajiri wao.”

Anasema kuwa shida ya mpango huu ni kuwa, hakuna aliyeporwa pesa zake kimabavu au kwa kushurutishwa, bali waliahidiwa kuwa pesa zao zingezalishwa na wawe matajiri na wakaingia kwa mtego na wakatoa pesa zao kwa matapeli hao kwa hiari.

“Tunasikia kuwa ukora huu unaweza kuwa umemeza zaidi ya Sh5 bilioni hapa nchini… Hatuna habari mwafaka na za kuaminika kuhusu kiwango halisi. Lakini ukikadiria zile Sh2.4 bilioni ambazo zilizama na Gakuyo na Ekeza kisha uongeze kampuni zingine tano zinazohusishwa na njama sawa na hiyo, tunakadiria kuwa kuna Sh5 bilioni au zaidi ambazo zimezama,” akasema.

Wabunge wa zamani

Wanaosemwa kuwa ndani ya kashfa hii ni pamoja na baadhi ya wabunge wa zamani na wengine walio nyadhifani kwa sasa, afisa mkongwe mstaafu katika huduma ya utawala wa kimaeneo na pia wafanyabiashara wakiwemo baadhi ya wachungaji.

Bw Rwagana Kariuki ambaye ni mwalimu mstaafu kutoka Kaunti ya Murang’a anasema kuwa alijipata katika ahadi sawa na hii ya kukusanya utajiri wa haraka.

“Nilipendezwa na ahadi kuwa baada ya miezi sita, hela zangu zote ambazo ningekuwa nimehifadhi katika moja ya kampuni hizi zingezalishwa kwa kuzidishwa kwa hadi mara sita… Nilichukua mkopo wa Sh500,000 kutoka kwa benki ya Equity na nikaongeza Sh400,000 zaidi kutoka akiba yangu na nikawapa wakurugenzi wa kampuni hiyo ya kikanisa,” anasema.

Aprili, aligundua kuwa wakurugenzi hao washahama kutoka kwa afisi zao katika Mji wa Murang’a na hata aliowajua na kupata namba zao za simu, hawazishiki akiwapigia.

“Ukweli ni kuwa nimepoteza pesa zangu…na sio mapeni, bali ni ukwasi halisi. Niko na mkopo wa benki na nimejifilisisha kwa kuwa akiba zangu zote niliweka kwa akaunti za hawa matapeli,” atafakari.

Anasema kuwa kwa sasa anasaka mteja wa kununua shamba lake la ekari 10 ambalo ataliuza kwa Sh15 milioni ili ajipe uthabiti tena wa kifedha.