Akili Mali

Jinsi biashara ya dera, vitenge na leso imempiga jeki kimaisha

June 11th, 2024 2 min read

NA CHARLES ONGADI

AKILI ni nywele kila mtu ana zake na mtafutaji hachoki akichoka basi ameshapata. Ndiyo kauli ya Khalfani Rukwaro, 33, mfanyabiashara maarufu wa vitenge, leso na dera mjini Mombasa.

Ni kati ya wafanyabiashara maarufu wa bidhaa hizi zinazopendwa sana na wakazi wa Pwani na hata bara wanaomiminika katika duka lake lililoko pembezoni mwa barabara ya Karisa Maitha, mkabala na Chuo cha Ualimu cha Shanzu, Kisauni.

“Tangu utotoni ndoto yangu ilikuwa ni kufanya biashara na wala si kuajiriwa na yeyote kutokana na msukumo unaotoka kwa matajiri wengi,” asema Khalfani wakati wa mahojiano na Akilimali majuzi.

Hata hivyo, kabla ya Khalfani kujitosa mzimamzima katika biashara hii, alilazimika kuajiriwa jijini Nairobi mara baada ya kukamilisha masomo yake ya Msingi mwaka wa 2002.

Licha kufaulu katika mtihani wa Darasa la Nane katika Shule ya Msingi, Khalfani hakuweza kuendeleza masomo yake ya Upili kutokana ukosefu wa karo.

Katika kuhakikisha anatimiza ndoto yake, alifululiza jijini Nairobi alikoajiriwa katika duka moja la kuuza vyakula tofauti alikohudumu kwa kipindi cha miaka mitatu.

Ni kipindi alichoweza kujiwekea mtaji uliomwezesha kufungua kioski kidogo eneo la Shanzu, Kisauni, Mombasa mwaka wa 2009.

“Nilianzia chini kwa kuuza bidhaa ndogo ndogo kama mkate, sukari, unga na bidhaa zengine katika kioski changu nikipata faida ila mambo yaliniendea segemnege mwaka wa 2020 wakati wa mlipuko wa virusi vya corona,” asimulia.

Kulingana na Khalfani, nusura akate tamaa baada ya biashara yake kuyumba kipindi cha mlipuko wa maradhi hayo.

Mkopo

Baada ya kutafakari, Khalfani aliamua kuchukua mkopo katika mojawapo ya kampuni za kukopesha kufufua upya biashara yake.

“Niliamua kufululiza hadi Moshi nchini Tanzania na kununua bidhaa mbali mbali kama vitenge, leso, dera, vyatu vya akina dada na marembesho mengine yanayotumiwa hususan na akina dada,” afichua.

Kwa mujibu wa Khalfani, biashara hii iliweza kufufua upya matumaini yake akipata wateja hususan akina dada wanaopenda aina ya dera maarufu kama ‘Bahawan’ iliyo na mtandio.

Vile vile, anasema anauza sana aina tatu za leso zinazovaliwa na wasichana na akina mama hasa wakati wa sherehe mbali mbali kama za harusi, posa, matanga na kadhalika.

Bei nafuu

Aidha, anakiri kinachowavutia wateja wake ni bei nafuu anayowauzia wateja wake huku Dera akiuza kuanzia Sh1,500 hadi Sh350 wakati leso zikianza kwa Sh800 hadi Sh350.

Khalfani anasema kabla ya biashara yake kuanza kunoga alikuwa akilazimika kusafiri hadi soko la Taveta ama Moshi Tanzania mara moja baada kwa mwezi kununua biadhaa hizi.

Lakini kwa sasa anaagiza bidhaa zake kutoka maeneo hayo mara mbili ama tatu kwa wiki kutokana na wateja kuongezeka na kumzidishia mapato yake ya kila siku.

Japo alidinda kufichua kiasi anachotia kibindoni kwa siku, alisema ni biashara ambayo imeweza kubadilisha maradufu maisha yake.

“Nimeweza kufungua duka lingine ambalo mke wangu anaendesha kutokana na faida niliyochuma kutoka kwa biashara hii mbali na kuanzisha miradi mingine mashambani (Taveta),” afichua.

Kulingana na Stephen Mumburi ambaye ni mfanyabiashara anayeuza bidhaa zake vijijini ni kwamba ananunua bidhaa zake katika duka la Khalfani kwa bei ya jumla kisha kuwazungushia wateja wake vijijini.

Stephen Mumburi mmoja kati ya wateja wa Khalfani akikagua aina tofauti ya leso katika duka lililoko katika barabara ya Karisa Maitha, Shanzu Mombasa. Picha|Charles Ongadi

Mumburi anasema aina ya leso, dera na vyatu vya akina dada anazonunua kutoka kwa duka la Khalfani ni za hali ya juu na zinazopendwa na wengi vijijini hususan maeneo ya Takaungu, Mnarani, Vipingo na Kaloleni Kaunti ya Kilifi.

Kati ya changamoto anazokumbana nazo ni baadhi ya wateja wake anaokopesha na kisha wanaingia mitini.

Aidha, anafichua siri ya mafanikio ni kuwa na nidhamu katika biashara huku akiwaasa vijana kuwa wabunifu katika kila wanalofanya kwa mafanikio ya baadaye.