Makala

Jinsi jamii ya Waluo inavyofunza Wapokot kula na kupenda samaki

June 20th, 2024 2 min read

NA OSCAR KAKAI

WAFUGAJI wanaoishi eneo la Kaskazini mwa Bonde la ufa hujivunia urithi na vyakula vyao vya kiasili. Vyakula vyao vya kila siku ni nyama, maziwa, damu na ugali kiasi.

Hata hivyo, kutokana na athari za kiangazi na mabadiliko ya tabia nchi katika kaunti ya Pokot Magharibi, wafugaji kwenye kaunti hiyo sasa wamekumbatia na kuzamia kula samaki.

Pokot Magharibi ni kati ya kaunti zenye kiwango cha juu cha utapiamlo kwa asilimia 35.1 kulingana na ripoti ya afya 2022 iliyofanywa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS) pamoja na Wizara ya Afya. Kaunti hiyo ni ya pili baada ya Kilifi kuwa na kiwango cha juu cha utapiamlo.

Hata hivyo, jamii ya Pokot imeanza kukumbatia kula samaki kama njia ya kuimarisha lishe na afya.

Kutokana na umaskini, uhaba wa chakula na masuala mengine kama utapiamlo kwa watoto, jamii za wafugaji sasa zimeamua kula samaki.

Jamii hizo za wafugaji zilijifunza haya kutoka kwa wenzao Waluo ambao ni wavuvi katika Ziwa Turkwel.

Zaidi ya watu 100 wa jamii ya Waluo ambao ni wavuvi wamepiga kambi katika kijiji cha Riting eneo la Turkwel.

Kulingana na wakazi wa Turkwel, walikuwa wakiona samaki kama nyoka na kuwa na mtazamo mbovu kuhusu samaki.

“Haikuwa rahisi. Tulikuwa tukifikiria kuwa samaki ni nyoka. Mimi binafsi nilibadilishwa na mwanaume Mjaluo ambaye alihakikisha kuwa ninapenda samaki,” anasema Dorine Loporinya, mkazi.

Kwa njia ya kukumbatia ulaji wa samaki, wameanza kubadilisha mlo wao.

“Nilifikiria nitatapika mara ya kwanza nilionja samaki lakini ikawa kinyume. Kwa sasa nimekuwa shupavu na hula samaki pamoja na mifupa yake yote,” anaelezea Bi Loporinya.

Bi Loporinya ambaye huuza samaki katika kituo cha kibiashara cha Riting anasema kuwa baada ya kuumia kutokana na kiangazi ambacho huua mifigo, wamekumbatia ulaji samaki.

Anasema kuwa sasa wamebadilika kutoka kwa maisha ya ufugaji na binafsi ana vyakula vya kutosha kwa meza na vingine vya kuuza.

“Hili limenisaidia pakubwa,” anasema.

Mama huyo wa miaka 42 anasema kuwa samaki imemsaidia kupata mapato na kuwa chakula kwa wanawe.

Mvuvi katika Ziwa Turkwel Peter Okoth ambaye alianza kazi hiyo 1994 anasema kuwa yeye ndiye aliwachochea wakazi kuanza kula samaki.

“Niliwafunza polepole jinsi ya kula samaki aina ya Salmon baada ya kuiita Moroy(Samaki),” anasema.

Anasema kuwa hatua hiyo imechangia vijana wengi kubadilisha mawazo yao kuhusu samaki na kuimarisha afya yao.

“Kwa muda mrefu eneo hili, ulaji wa samaki hakushabikiwa wakisema samaki ina harufu mbaya,” anasema.

Charles Otiende, mvuvi mwingine anasema kuwa watu wengi wa eneo hilo wameanza maisha mapya.

“Walikuwa wakilala nja ilihali kuna samaki wengi ambao wanaoza,” anasema.

Naibu wa chifu wa kata ya Kostei Joseph Siwa anasema kuwa kaunti hiyo inakumbwa na hatari ya kiangazi ambayo huathiri wakazi.

“Wakati wa kiangazi watu hanunua chakula kwenye soko, sababu mbuzi wote wamekonda. Lakini samaki ni tofauti. Samaki wanahitaji tu maji na kushika samaki kubwa huwezesha familia kupata chakula cha kutosha. Kwa sasa kuna watu wengi ambao wamekubali kula samaki na hata kufanya biashara za kuwapatia mapato.

Ziwa Turkwel limekuwa kituo cha kuzalisha samaki wengi baada ya mamlaka ya ustawi wa  eneo la Bonde la  Kerio (KVDA) na serikali ya kaunti kuanza kutekeleza mipango ya uvuvi kama njia ya kuongeza mapato kwa wakazi na kuimarisha lishe, mpango ambao umesaidia katikautoshelevu wa chakula na lishe bora.

Meneja Mkurugenzi wa KVDA Sammy Naporos anasema kuwa wameongeza samaki wengi kwenye bwawa la Turkwel ambao wanazaana.