Makala

Jinsi kaunti ya Kisii inavyokabili corona

July 14th, 2020 2 min read

Na LYDIA OMAYA

KISA cha kwanza cha corona katika kaunti ya Kisii kiliripotiwa Machi na hadi sasa visa vimefikia sita.

Watano kati ya sita hao wamekwisha pata nafuu na wakaruhusiwa na kurejea nyumbani.

Mmoja bado anahudumiwa katika chumba cha kutengwa. Kufwatiliwa kwa wale waliotangamana na wagonjwa kunaendelea ili kudhibiti msambao.

Idadi ya visa hivi si kubwa na hivyo basi ni dhahiri kwamba kaunti ikijizatiti vitaisha.

Kuna mwongozo ambao umetolewa katika kaunti hii unaosababisha visa kuwa vichache.

Bila mwongozo huu huenda visa vikaongezeka na kusambaa kwa haraka mno na hivyo basi idadi kuongezeka.

Baadhi ya mambo yaliyo katika mwongozo huo ni msisitizo wa kuvaa barakoa, kuwa mbali hasa kati ya mtu na mwenzake, kuosha mikono kwa kutumia sabuni na hata kukaa nyumbani.

Siku zilizopita mambo haya yamekuwa yakizingatiwa na wakaaji wa Kisii na ndiposa visa vikawa vichache.

Ikiwa kila mmoja atafahamu na kuelewa fika sheria na mwongozo huu upo kwa usalama wa mtu binafsi,basi watu wote watawajibika kukomesha corona katika kaunti hii ya Kisii.

Wizara ya Afya ya Kaunti ya Kisii ikiongozwa na Bi Sarah Omache inatumia njia nyingi kuhamasisha wakazi wa eneo hili namna ya kujikinga dhidi ya janga hili la Covid-19 kwa kuwa “kinga ni bora kuliko tiba.”

Mojawapo ya njia hizo ni kuweka matangazo ya kila mara kwenye vituo vya redio vinavyolenga hadhira ya Kisii na kusikilizwa eneo hili.

Matangazo hayo yanasisitiza mwongozo unaotolewa na Wizara ya Afya na hata pia kujulisha watu jinsi virusi hivi vya corona vinavyosambaa.

Heri kutahadhari kabla ya hatari kwa sababu visa vikiongezeka huenda ikawa vigumu kukabili corona.

Kuna vituo vya kutengwa katika kila kaunti ndogo na pia katika hospitali ya Kisii Training and Referral Hospital ni mojawapo ya kituo ambapo kuna vitanda 318 vimewekwa tayari kwa ajili ya wagonjwa watakaopatikana na corona.

Bi Omache anasema wahudumu wa afya wote katika kaunti pamoja na wale 100 ambao waliongezwa na serikali kuu wamepokea mafunzo ya jinsi ya kushughulikia visa vya corona vitakapotokea; yaani namna ya kushughulikia wagonjwa.

Ingawa hivyo, wahudumu bado hawatoshi na ikiwa idadi ya visa itaongezeka zaidi, basi huenda huo utakuwa mwanzo wa majonzi.

Kwa jitihada za serikali ya Kaunti ya Kisii wahudumu hawa wa afya wamekabidhiwa vifaa tokea mavazi ya kujikinga dhidi ya corona – PPE – hadi vifaa vya kupima wakazi wa kaunti hii ijapokuwa pia ni vichache.

Ni jambo la kuridhisha wakazi wa Kisii kuona serikali ya kitaifa na ile ya kaunti zikishirikiana pakubwa aghalabu katika bajeti ya afya ili kukabili corona.

“Serikali ya kitaifa ilitupa zaidi ya Sh100 milioni na kwa hakika fedha hizo zimesaidia pakubwa katika pambano hili,” Bi Omache akasema.

Ili kuwa na vitanda 300 kuendana na wito wa alivyoagizwa Rais Uhuru Kenyatta, kaunti inajizatiti.

Lakini haikuwa rahisi. Ndiposa serikali ya kaunti inazidi kujikaza. Si vitanda tu bali hata vifaa vingine vya kufanyia vipimo vya kimatibabu, barakoa zaidi ya 500,000 na mitungi ya maji na sabuni pia imepeanwa kwa umma ili kuhakikisha usalama wa kila mmoja.

Huku wengine wakijizatiti kufuata mwongozo uliotolewa na Wizara ya Afya, baadhi ya wakazi wa Kisii hawaoni umuhimu wowote “kwani afya ni baraka ya Rabuka.”

Wanasahau kuwa amri zipo kwa usalama wa kila mtu binafsi. Hata hivyo, wanaojaribu kukiuka sheria hizo kama vile kuvaa barakoa ipasavyo wanadadisiwa. Ili kuhakikisha kaunti ya Kisii inazuia maambukizi zaidi, basi jambo la leo haliwezi likangoja kesho.