Bambika

Jinsi Khalwale alivyotegua kitendawili cha familia pana

February 9th, 2024 2 min read

NA MARY WANGARI

SENETA wa Kaunti ya Kakamega Boni Khalwale amezua gumzo nchini baada ya kuwatambulisha wake zake wanne akiwemo yule aliyeaga dunia.

Dkt Khalwale ambaye ni mbunge wa zamani wa Ikolomani vilevile alikiri kujivunia kuwa baba wa watoto 17 aliojaaliwa pamoja na mabibi hao wake.

Akihutubia vyombo vya habari baada ya hafla ya mazishi ya mfanyakazi wake, Kizito Amukune Moi, seneta Khalwale alifichua kuwa mke wake wa kwanza, Adelaide Khalwale, aliaga dunia mnamo 2019.

Wake wengine wa seneta huyo ni pamoja na Josephine Umina (mke wa pili), Gloria, Sekeiyan (mke wa tatu), na Diana Moragwa, mke wa tatu, alifichua Seneta huyo wa Kakamega.

Katika kinachoonekana kama juhudi za kupuuzilia mbali madai kuwa mmoja kati ya wake zake alikuwa na mahusiano nje ya ndoa kiasi cha kuzaa na mwanamme mwingine, Seneta Khalwale alisisitiza kuwa watoto wake wote wanafanana naye.

“Wake nilio nao, ninawafahamu vyema na ni kama wafuatavyo, wa kwanza, Adelaide Khalwale aliyeaga dunia miaka mitano iliyopita,” alisema Dkt Khalwale.

“Ni mama ya watoto wangu watatu wa kwanza. Wote wanaofanana nami kama shilingi kwa ya pili, hakuna shaka kuhusu nani ndiye baba yao mzazi.”

“Josephine Khalwale, mke wangu wa pili, ndiye mama wa watoto wangu wa tatu, mmoja ambaye amekamilisha elimu ya chuo kikuu na wengine wawili ambao wangali chuo kikuu. Wote wanafanana nami, hakujakuwa na malalamishi yoyote kuhusu hilo.”

“Wa tatu ni Gloria Khalwale, ambaye ni mama wa watoto wangu wanane, miongoni mwao, baadhi wako chuo kikuu wengine wako viwango vya chini vya elimu. Wote tunafanana na hakujawahi kuwa na shaka kuhusu baba yao mzazi.”

“Mwisho, Diana Khalwale, mama ya watoto watatu, wote walio katika viwango vya chini vya elimu. Watoto hao wote wanafanana nami.”

Hatua ya seneta Khalwale huenda ilichochewa na madai yaliyotolewa na mfanyabiashara wa Kakamega Cleophas Shimanyula almaarufu Toto, kuwa mwanasiasa huyo alimuua mfanyakazi wake Kizito.

Hata hivyo, ripoti za upasuaji uliofanywa mara mbili kando kando mnamo Januari 29, 2024, na Februari 3, 2024, zilithibitisha kuwa mfanyakazi huyo wa Bw Khalwale aliaga dunia baada ya kushambuliwa na fahali wa bosi wake.

Ripoti hizo zilitolewa na Mpasuaji wa eneo la Magharibi, Dkt Dickson Muchana na mpasuaji wa serikali Dkt Johansen Oduor.

Hatua ya seneta Khalwale kufungua moyo kuhusu familia yake huenda sasa ikawapa jibu Wakenya ambao wamekuwa wakishangaa kwa nini muundasheria huyo amekuwa akishereheke karibu kila wakati, matokeo ya watahiniwa wenye jina lake kwenye mitihani ya KCPE na KCSE karibu kila mwaka.