Bambika

Jinsi Kizungu cha Gachagua kilivyofanya warembo kummezea mate

May 21st, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI 

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amefichua kwamba enzi zake katika shule ya upili alikuwa akijishindia warembo kupitia kuongea Kiingereza sanifu kupitia kwa pua.

Aidha, wakati wa mijadala katika ukumbi wa mijadala shuleni, alikuwa akipamba Kizungu chake kwa kila aina ya mbinu na kuongea kwa ufasaha, hatua hiyo ikiwaacha vinywa wazi wanafunzi wa kike.

Alisema bidii ya walimu wake ndio ilimpa raha hiyo ya kunoa bongo lake hadi kumwezesha kuwa ‘Mzungu Mweusi’.

Bw Gachagua ni miongoni mwa wanasiasa nchini ambao ufasaha wao wa lugha ya Kiingereza na ulumbi wake husisimua wapenda lugha na fasihi.

Kiongozi huyo aliongeza kwamba kwa sasa “lau si bidii ya walimu wangu kuninyorosha, mimi ningekuwa nimekunywa pombe haramu hadi kuangamia”.

“Daima dawamu nitaishi kuwatambua walimu kwa kuwa isipokuwa ni wao, yangu yangekuwa mengine. Singeishi kuwa mimi wa leo. Ningezama kwa maovu ya kila aina. Kila mmoja wetu akifanikiwa, amkumbuke mwalimu wake na ikiwezekana, ‘mchinjie nyama kusema ahsante’,” akasema Bw Gachagua.