Makala

Jinsi Lizzie Wanyoike alivyojizolea ukwasi kutoka mshahara wa Sh900 hadi bilionea

January 17th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

SAFARI ya mwanzilishi wa Nairobi Institute of Technology and Business Studies (NIT-BS) marehemu Lizzie Wanyoike ilianza kushika kasi mwaka wa 1999 licha ya kwamba ilikuwa katika ratiba tangu 1979.

Alikuwa ametoka kwa ndoa yake na aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Mburu Wanyoike na ambaye kwa pamoja walikuwa wakiendesha taasisi ya Temple College of Secretarial Studies.

Lizzie ambaye alikuwa mwalimu na karani kitaaluma, kabla ya mauti yake alikuwa ameambia Taifa Leo kwamba alikuwa ameajiriwa kama mwalimu akilipwa mshahara wa Sh900 kwa mwezi mwaka wa 1975 lakini akajiuzulu ili kukoleza ladha ndoa yake mara tu yeye na Bw Wanyoike walipofunga pingu za maisha.

Alikuwa mwalimu katika Shule ya Upili ya Wasichana ya State House Girls, Nairobi.

Alipotoka kwa ndoa, alionelea azindue shule yake ya kitaaluma na ndipo Nairobi Institute of Business Studies (NIBS) ilianza jijini Nairobi ikiwa na wanafunzi 25 ambao aliwanunua kutoka kwa taasisi nyingine ambayo ilikuwa imelemewa na kuendelea kutoa huduma.

“Kwa kuwa nilitoka kwa ndoa yangu bila chochote, niliuza ploti kadha ambazo nilikuwa nimejinunulia kwa jina langu na pia nikachukua mkopo kutoka kwa benki. Mungu alikuwa nami kwa kuwa biashara hiyo ilipata neema na ikastawi kwa haraka,” akasema wakati huo.

Lizzie Wanyoike (kulia) wakati wa uhai wake alipopigwa picha pamoja na bintiye Stella katika tuzo za mwekezaji bora wa 2018. PICHA | MWANGI MUIRURI

Licha ya kuandamwa na changamoto kadha kama za upangaji huku wanafunzi wakizidi kuwa wengi, alinunua shamba la ekari 10 katika mtaa wa Kimbo ulio viunga vya mji wa Ruiru na akajenga makao makuu ya taasisi hiyo.

“Mwaka wa 2015 nilikuwa natazamia kuigeuza kuwa chuo kikuu lakini nikaonelea nizingatie kozi za kiufundi na ndipo tukabadilisha jina hadi NIT-BS,” akasema.

Kabla ya kukumbana na mauti mnamo Januari 14, 2024, akiwa na umri wa miaka 73, Lizzie alikuwa amepanua biashara hiyo hadi kuwa na wanafunzi 7,038 katika jiji kuu la Nairobi na katika maeneo ya Ngong’, Ruiru, na Nakuru huku akiwa pia amezindua shule ya msingi ya Lizzie Wanyoike Preparatory.

Aidha, alikuwa amezindua biashara ya hoteli ya Emory jijini Nairobi.

Alisema kwamba alikuwa ameweka msingi thabiti wa uwekezaji wake kupitia kuwaweka watoto wake watatu ndani ya usimamizi wa miundombinu, operesheni na pia katika vitengo vya kifedha.

[email protected]