Habari Mseto

Jinsi Lizzie Wanyoike alivyoogopa kuparara

January 17th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

MWEKEZAJI Lizzie Wanyoike aliyeaga dunia mnamo Januari 14, 2024, akiwa na umri wa miaka 73 alikiri kwamba aliolewa mapema ili kuhepa hatari ya kurejea mashambani kuparara.

“Punde tu baada ya kumaliza kozi yangu ya ualimu na ukarani katika Taasisi ya Kenyatta, sasa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU), niliingia moja kwa moja kwa ndoa ambayo ilikuwa na watoto wa kambo watatu. Kulikuwa na mke mwingine ambaye alikuwa amemhepa mzee wangu,” alisema katika kitabu cha maisha yake ambacho alikuwa ananuia kukichapisha.

Aliyemuoa alikuwa kwa wakati huo ni Mburu Wanyoike ambaye alikuwa mkurugenzi katika shirika la maziwa la KCC.

Wanyoike ambaye kwa sasa naye pia ni marehemu, alikuwa amemzidi umri kwa zaidi ya miaka 10.

“Baada ya kulelewa mashambani na kushuhudia shida za huko moja kwa moja, nilikuwa sasa jijini kusoma na nikaona maisha tofauti yaliyokuwa na mwangaza. Hakuna vile ningekubali kurejea huko kijijini kuparara,” akasema.

Bi Wanyoike alingia katika ndoa hiyo bila mkataba wowote “na nilimtazamia mume wangu kama babangu na mlezi hali ambayo baadaye ilianza kutatiza ndoa yetu”.

Katika pendekezo la kitabu hicho chake mwaka wa 2019, alikiri kwamba hali ingejirudia tena akiwa na ufahamu aliokuwa amepata katika ndoa hiyo, hangekimbilia ndoa ili kuepuka shida.

“Nusura hata mimi nizame katika masaibu yaliyonifuata,” akasema.

Bi Wanyoike alisema aliona dalili za macho ya kumsuta kuwa mgeni katika boma la mumewe huyo lakini akajifariji kuwa hali kama hiyo kwa asilimia kubwa hutokea kwa ndoa za aina hiyo.

“Mimi niliingia katika ndoa na nikawa mama moja kwa moja wa watoto watatu wakubwa. Licha ya kuwa bwanangu alikuwa ananipenda na kunipa mahitaji yangu yote, bado nilijipata nikiwa na etieti jinsi nilivyozidi kupevuka kimaisha,” akasema.

Katika hali hiyo, licha ya bwanake kufanikiwa kimaisha na kuwa mbunge wa Gatanga kati ya 1992 na 1997, haja ya talaka ilitanda na katika uamuzi wa mahakama, Lizzie alitemwa nje hata ya urithi akiambiwa hakuwa mke halali kwa kukosa mkataba wa ndoa.

Bw Wanyoike alikuwa ameanza kuwania ubunge huo mwaka wa 1979 bila mafanikio na hatimaye akaunasa mwaka wa 1992.

“Mimi niliondoka katika ndoa hiyo nikiwa na nguo nilizokuwa nimevaa mwaka wa 1998 na katika mahangaiko makuu ya kupoteza maisha ya kifahari, nikaanza kujijenga upya huku nusura nisombwe na mawazo hadi kuwa kichaa,” akasema.

Na hapo ndipo safari yake ya kuwa bilionea tajika ilianza, huku akiruka visiki chungu nzima hadi wakati wa kifo chake ambapo alikuwa amejijengea jina, familia, mali, na historia.

[email protected]