Makala

Jinsi maiti ya mwanamke wa Kiislamu inavyoandaliwa kipindi hiki cha janga la Covid-19

August 16th, 2020 2 min read

Na FARHIYA HUSSEIN

MUUMINI wa dini ya Kiislamu akifariki, mwili wake unapaswa kuoshwa na kutayarishwa na wanafamilia wa jinsia sawa na aliyefariki ambapo baadaye yeye huzikwa na wanaume.

Lakini tangu kuzuka kwa janga la kirusi cha korona – corona – ibada za mazishi za ulimwengu zimebadilika sana.

Kwa mfano, sasa miili ya Waislamu haipaswi kuoshwa wala kusafirishwa kwa jeneza; hali ambayo ni kinyume na sheria za dini hiyo.

Kulingana na Mwenyekiti wa Kamati ya Waislamu inayosimamia Mazishi Mombasa, Sheikh Rishaad Rajab, katika sheria za Kiislamu – sharia – maiti inastahili kuoshwa kwanza kabla ya mazishi.

Kwa kawaida, mwanamume akifariki huoshwa na wanaume nao wanawake hushughulikiwa na jinsia ya kike lakini sasa mambo hayafanywi hivyo; wengi wakizingatia yale kamati ya afya imeainisha kama njia mojawapo ya kutosambaza kirusi cha korona.

“Hivi sasa miili haioshwi kama inavyostahili katika sharia ya Kiislamu. Pia, hatutumii tena jeneza kwa sababu kwa sisi Waislam kawaida tunasafirisha miili hiyo kwa kutumia jeneza moja ambalo ni mali ya msikiti,” anasema Bw Rajab.

Anaongeza kuwa katika hali zingine, ikiwa familia itaomba mtu wao kusafirishwa akiwa amewekwa kwa jeneza, basi hili linafaa kufanywa kupitia njia za kuzuia kusambaa kwa kirusi.

Mfano mzuri ni mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Changamwe, Ramadhan Kajembe ambaye familia yake iliiomba awekwe katika jeneza na kusafirishwa.

Kuhakikisha itifaki za afya zinazingatiwa na kufuatiwa kwa dhati, miili ya wanawake wa Kiislamu sasa inaandaliwa na kamati iliyochaguliwa inayoacha familia nyingi nje ya mpango wa mazishi.

Bi Asia Sunkar ambaye pia ni katibu wa kamati hiyo anafafanua kuwa kwanza wanapokea simu kutoka kwa hospitali au nyumba ambayo mwanamke amekufa, kisha wanavaa kikamilifu na kujikinga wakitumia mavazi spesheli – PPE – ili kuushughulikia mwili.

Kulingana na yeye wakati visa vya mwanzo kabisa za kirusi cha korona ziliripotiwa nchini, waliona umuhimu wa kuwa na kamati ambayo itasaidia familia zitakazopata changamoto za mazishi.

“Kwanza tunapokea simu kutoka kwa hospitali au nyumba ambayo marehemu amekataa roho, halafu wawili wetu tunatembelea eneo hilo tukiwa tumevalia PPE,” anafafanua.

Wakisimamiwa na msimamizi mmoja wa afya, wanaanza mchakato kuhakikisha familia hazikaribii mwili wa mwendazake.

“Tunatumia shuka mbili nyeupe kufunika mwili kisha baadaye tunaweka ndani ya Mifuko ya Mwili ambayo itakuwa tayari kwa usafirishaji,” muuguzi Bi Sunkar anasema.

“Mara tu tunapomaliza kuandaa maiti, kamati ya wanaume huja na kuuchukua mwili kwa maziko. Hii ni kwa sababu katika Uislamu wanawake hawaruhusiwi kuhudhuria maziko eneo la kaburi hata ikiwa ni ya familia,” anasema Bi Sunkar.

Ingawa hivyo, wao kama kamati pia wanakabiliwa na changamoto.

“Hatuna mdhamini, kwa hivyo tunachanga pesa wenyewe ili kununua glavu na PPE. Pia hatuwezi kuzirudia kwa hivyo baada ya kushughulikia mwili tunatupa PPE na zinachomwa. Wakati mwingine tunaomba gari ambalo litasafirisha mwili ili kusaidia familia ikiwa haina pesa za kutosha kushughulikia mazishi, “anasema.

Kamati hiyo imeshirikiana na Serikali ya Kaunti ya Mombasa na imeanza kufanya mazoezi ya kuajiri wanachama zaidi kwa matumaini ya kuenea katika mwambao wa Pwani.

“Tunawafundisha baadhi ya wanachama wetu katika Hospitali ya Mewa kuhusu suala la saikolojia na hata jinsi ya kukaa salama wakati wa kushughulikia mwili ili wasipate maambukizi ya kirusi cha korona,” akasema Bi Sunkar.

Kufikia sasa wamefanya mafunzo hayo na hamasisho katika kaunti ndogo kadhaa zikiwamo Changamwe, Kisauni, Jomvu na Bamburi.