Habari Mseto

Jinsi mfanyabiashara alivyosambaratishiwa kiwanda kwa kupewa bili kubwa ya stima kimakosa

April 6th, 2024 1 min read

Na EVANS JAOLA

MFANYABIASHARA wa Kaunti ya Trans Nzoia alilazimika kufunga biashara aliyotumia Sh10 milioni kuanzisha baada ya kulimbikiziwa bili ya stima ya Sh417, 972 kimakosa na kampuni ya Kenya Power.

Paul Njuguna Mwangi 65, anasema biashara yake ya kuzalisha mafuta ya kupikia ilikuwa ikifanya vyema hadi Agosti 2021 alipopokea bili hiyo kutoka kwa Kenya Power ikidai ilikuwa ya kampuni yake ndogo.

Biashara yake iliporomoka alipokatiwa stima na KPLC Novemba 2021.

Aliwasilisha kesi katika jopo la kuamua mizozo ya kawi na petroli.

Katika uamuzi uliotolewa Machi 26, 2024 na mwenyekiti wa jopo hilo Bi Doris Kinya Mwirigi, alisema kuwa mlalamishi alikosa stima kwa miezi minane kwa makosa ya mshtakiwa wa kwanza ambaye ni KPLC na wa pili ambaye ni Mamlaka ya Kawi na Petroli na kwamba kampuni haikutimiza viwango vyake vya ubora katika utoaji huduma.

Jopo lilimwagiza asilipe bili ya Sh417,972.

Bw Mwangi sasa anataka alipwe fidia ya Sh2.4 milioni kwa hasara aliyopata baada ya kukatiwa stima kwa miezi minane.

”Nilikuwa nikipata Sh300,000 kwa mwezi kabla ya kukatiwa stima lakini sasa nipata karibu Sh100,000 kumaanisha biashara iliporomoka na ndio sababu ninataka fidia kutoka kwa serikali niweze kufufua biashara yangu,” aliambia Taifa Leo kwenye mahojiano.