Makala

Jinsi Moi alivyowakabili wapinzani na wakosoaji wake

February 4th, 2020 4 min read

Na WANDERI KAMAU

HAYATI Rais Mstaafu Daniel Moi atakumbukwa kwa kuwakabili vikali wale ambao walikosoa utawala wake.

Bw Moi hakujali ikiwa waliomkosoa walikuwa washirika wake wa karibu au la.

Miongoni mwa wale waliojikuta kwenye mkwaruzano wa kisiasa na Bw Moi ni Mwanasheria Mkuu wa zamani Charles Njonjo, mfanyabiashara Andrew Muthemba, wanachama wa kundi la Mwakenya, kiongozi wa ODM Raila Odinga, mwanasiasa Kenneth Matiba, Kasisi Timothy Njoya miongoni mwa wengine.

Masaibu ya Bw Njonjo yalianza kwenye mkutano mmoja wa Bw Moi Kaunti ya Kisii mnamo 1983.

Kwenye ziara katika eneo hilo, Bw Moi alisema kuwa baadhi ya nchi za Magharibi zilikuwa zikipanga kumsaidia mmoja wa “wasaliti wake” (Njonjo) kutwaa uongozi.

Kilichofuatia ni njama za kumhangaisha Bw Njonjo, wakati huo akihudumu kama Waziri wa Masuala ya Kikatiba.

Mahasimu wake wa kisiasa waliungana kumtaja kuwa “msaliti.”

Njonjo alijitosa siasani mnamo 1980 baada ya kustaafu kama Mwanasheria Mkuu.

Alitumia washirika aliobuni akiwa Mwanasheria Mkuu na ukaribu wake na Bw Moi kujijenga kama mojawapo ya wanasiasa wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini.

Kwenye harakati hizo, alipata mahasimu wengi, kulingana na kitabu Moi: The Making of an African Statesman kilichoandikwa na Bw Andrew Morton.

Hatua ya Bw Njonjo kujitosa kwenye siasa pia ilizua uhasama kati yake na Rais Mstaafu Mwai Kibaki, aliyekuwa Makaku wa Rais.

Muda mfupi baada ya mkutano wa Kisii, mbunge wa Kericho ya Kati Francis Mutwol, alimtaja Njonjo kuwa “msaliti aliyepania kutwaa mamlaka kama rais, hata bila ya kuhudumu kama waziri.”

Kilichofuatia kilikuwa msururu matukio ya kumhangaisha Bw Njonjo, hali iliyomfanya kujiuzulu kama Waziri na Mbunge.

Bw Moi alibuni tume maalum ya kumchunguza mnamo Julai 1983, ambapo alipatikana na hatia.

Mnamo Juni 29, 1983, mbunge wa Butere Martin Shikuku aliwasilisha stakabadhi Bungeni akidai kwamba Bw Njonjo alimiliki biashara za siri nchini Afrika Kusini, na alikuwa ameingiza silaha hatari nchini kinyume cha sheria ili kuipindua serikali.

Licha ya kupinga madai hayo, Bw Njonjo aliondolewa serikalini na tume maalum iliyobuniwa ili kumchunguza.

Siku iliyofuata, aliondolewa kutoka chama cha Kanu, hali iliyomfanya kujiuzulu kama mbunge.

Mnamo Julai 1983 Bw Moi aliivunja Bunge mapema na kuandaa uchaguzi mnamo Septemba ili kuwaondoa wanasiasa walioonekana kumuunga mkono Bw Njonjo.

Licha ya kupatikana na hatia na tume hiyo mnamo 1984, Bw Moi alimsamehe Bw Njonjo. Hata hivyo, ushawishi wake siasani ulipungua kabisa.

Andrew Muthemba

Mnamo Machi 19, 1981, Wakenya waliamkia habari kwamba mfanyabiashara Andrew Muthemba kutoka Nairobi amekamatwa na kufunguliwa mashtaka kuhusu njama za kuipindua serikali.

Kulingana na mashtaka, Bw Muthemba alituhumiwa kwamba kati ya Desemba 15, 1980, na Februari 23, 1981, alikuwa “amedhamiria na kupanga njama za kumpindua Bw Moi kama Rais wa Kenya.”

Mashtaka dhidi ya Bw Muthemba yalijiri wakati Bw Moi alikuwa mwenye hofu kuhusu njama za kumwondoa mamlakani.

Mnamo Aprili 1980, alikuwa ameonya kwamba angewakamata wale waliokuwa wakipinga utawala wake na kuwaweka gerezani.

Kilichojulikana ni kuwa kati ya Desemba 15, 1980 na Februari 23, 1981, Bw Muthemba alikuwa amejaribu kupata usaidizi wa Koplo Joseph Njiru kuiba grunedi kumi na mabomu kadhaa.

Vilevile, alikuwa amejaribu kuomba msaada wa Kapteni Ricky Waithaka kuiba grunedi 100 kati ya silaha zingine za vita.

Katika kujitetea kwake, Bw Muthemba alimwambia Hakimu Fidahussein Abdullah kwamba “alikuwa akitekeleza majukumu yake kama kawaida.”

Polisi hawakuamini kauli yake.

Bw Muthemba alisema kwamba alikuwa akichunguza utoaji wa vibali vya kufanyia kazi kwa raia wa kigeni nchini kinyume cha sheria kwa ufahamu wa Bw Njonjo, aliyehudumu kama Waziri wa Masuala ya Kikatiba.

Serikali ya Moi ilianza kuwa yenye tashwishi kutokana na uhusiano wa karibu kati ya mfanyabiashara huyo na Bw Njonjo.

Kwa kumtaja Njonjo kwenye kesi yake, Muthemba alitumaini kwamba angemsaidia kujitoa kwa masaibu yaliyomkumba. Hata hivyo, hakufahamu kwamba Bw Njonjo pia alikuwa amelengwa na serikali ya Moi.

Ingawa kesi yake ilisikilizwa na kufutiliwa mbali baadaye, Bw Muthemba alisisitiza kuwa maafisa wote wakuu serikalini walifahamu kuhusu harakati zake za kutaka kuchunguza utoaji vibali vya kufanyia kazi nchini. Alidai kusalitiwa kwa kuwa jamaa wa Bw Njonjo.

Mwakenya

Baada ya kuifanya Kenya kuwa nchi ya chama cha Kanu pekee kufuatia jaribio la mapinduzi mnamo 1982, wanaharakati nchini walibuni kundi la Mwakenya (Muungano wa Wazalendo wa Kenya) ulioegemea mfumo wa utawala wa ujamaa.

Muungano huo uliwashirikisha wanahabari, wahadhiri, viongozi wa kidini na wanasiasa. Kundi hilo lilimlaumu Moi kwa maovu kama ufisadi, ukabila na ubadhirifu wa fedha za umma.

Wanaharakati hao pia walimtaka Bw Moi kurejesha mfumo wa vyama vingi nchini kwa kukifanyia mageuzi kipengele 2 (a) cha Katiba.

Msemaji wake mkuu alikuwa mwandishi maarufu wa vitabu Prof Ngugi wa Thiong’o.

Muda mfupi baada ya jaribio hilo, Shirika la Ujasusi (Special Branch) lilianza operesheni kali ya kuwakamata wale waliodaiwa kushiriki.

Waliokamatwa kwanza ni mhadhiri Maina wa Kinyatti, Prof Katama Mkangi, mwanasiasa Wanyiri Kihoro na Paddy Onyango.

Wengine waliokamatwa ni Kiongo Maina, Mwandawiro Mghanga, mwandishi Wahome Mutahi, Lumumba Odenda na Oduor Ong’wen.

Wengi wao walikamatwa na kufungwa gerezani bila kufunguliwa mashtaka. Wengine walidhulumiwa katika majumba ya dhuluma ya Nyayo na Nyati jijini Nairobi.

Bw Moi aliwaambia Wakenya kwamba wanachama wa muungano huo hawakuwa Wakenya, bali wasomi na wanaharakati ambao walikuwa wakiendeleza ajenda na maslahi ya nchi za kigeni.

Alisema kuwa wote walikuwa na paspoti ambapo wangetoroka nchini mara tu serikali ingeanza kuwakabili.

Mnamo 1992, mama za wanaharakati kutoka eneo la Kati ambao wanao walikuwa wamekamatwa kwa kujihusisha na kundi hilo walikusanyika katika Bustani ya Uhuru Park jijini Nairobi, wakimtaka Bw Moi kuwaachilia.

Miongoni mwa waliokuwepo ni Mshindi wa Tuzo la Nobel marehemu Wangari Mathai na Bi Monicah Wangu, mamake aliyekuwa mbunge wa Subukia Bw Koigi wa Wamwere.

Serikali ya Moi iliwatuma maafisa wa usalama kuwatawanya. Hata hivyo, walilipiza kisasi kwa kutoa nguo zao zote. Kufikia Julai 1993, wanaharakati wote walikuwa wameachiliwa.

Raila Odinga

Bw Odinga aliwekwa kizuizini nyumbani kwake baada ya ushahidi wa mwanzo kuonyesha kuwa alishirikiana na wale waliopanga jaribio la mapinduzi mnamo 1982 dhidi ya Bw Moi.

Baadaye, alifunguliwa mashtaka ya uhaini na kufungwa miaka sita gerezani bila kufunguliwa mashtaka.

Aliachiliwa mnamo Februari 1988 lakini akakamatwa tena mnamo Septemba mwaka uo huo.

Aliachiliwa mnamo Juni 1989 lakini akakamatwa tena mnamo Julai 1990 pamoja na mwanasiasa Kenneth Matiba na mwenzake Charles Rubia.

Matiba na Rubia

Chini ya maagizo ya Bw Moi, Bw Matiba alifungwa gerezani bila kufunguliwa mashtaka yoyote katika Gereza la Kamiti pamoja na Bw Rubia.

Wawili hao walishtakiwa kwa kushinikiza mageuzi ya Katiba ili kuruhusu uwepo wa vyama vingi ya kisiasa.

Akiwa gerezani, Bw Matiba alinyimwa nafasi ya kutibiwa, hali iliyomfanya kuugua kiharusi hadi kufariki kwake mnamo 2018.

Njoya na Muge

Serikali ya Bw Moi pia iliwakabili vikali viongozi wa kidini ambao walitumia nafasi na ushawishi wao kuikosoa.

Miongoni mwa wale ambao walijipata pabaya ni Kasisi Timothy Njoya wa Kanisa la PCEA, Askofu Alexander Kipsang Muge wa Kanisa la Anglikana (ACK) miongoni mwa wengine.

Njoya alikuwa mmoja wa viongozi wa maandamano ya Sabasaba mnamo Julai 7, 1990, yaliyoshinikiza kuanzishwa kwa mfumo wa vyam vingi nchini.

Hata hivyo, Njoya alikamatwa na kupigwa vibaya na polisi, kwa kushiriki kwenye maandamano hayo.

Naye Askofu Muge alifariki katika hali tatanishi mnamo Agosti 14, 1990, muda mfupi baada ya kuonywa na aliyekuwa Waziri wa Leba Peter Okodo dhidi ya kwenda Busia.

Hadi sasa, chanzo cha kifo chake hakijawahi kubainika.