Makala

Jinsi mti aina ya Mpeketo ulivyomfanya Jomo Kenyatta kupenda Lamu

March 16th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

MAPENZI aliyokuwa nayo mwanzilishi wa taifa hili, hayati Mzee Jomo Kenyatta kwa Lamu yalimsukuma kiongozi huyo wa taifa kuzuru eneo hilo na kuacha alama au kumbukumbu ya milele.

Mnamo miaka ya sabini (1970s), Mzee Kenyatta alifika katika eneo mojawapo la Lamu lililotambulika kwa jina la asili kama Ziwa Mkunguya.

Ni hapa ambapo Mzee Kenyatta, katika harakati za kutafuta upepo mzuri wa kubarizi, alifika palipokuwa na mti mmoja kwa jina Mpeketo.

Kiongozi huyo alikaa chini ya kivuli chake na kupenda mandhari hayo si haba.

Ilimlazimu kiongozi huyo wa taifa kuagiza chakula cha mchana alichokuwa ameandaliwa kifikishwe mahali alipobarizi ambapo alikula papo hapo.

Punde alipomaliza kula na kushiba, Mzee Kenyatta aliuliza wenyeji jina halisi la mti huo uliomsitiri kwa kivuli chake kizuri.

Alipoambiwa mti huo unaitwa Mpeketo, Mzee Kenyatta alicheka na kisha kuagiza kwamba kuanzia wakati huo eneo hilo zima la Ziwa Mkunguya libadilishwe jina na kuitwa Mpeketoni.

Sehemu mojawapo ya mji wa Mpeketoni, Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Hivyo ndivyo mji wa Mpeketoni ulioko Kaunti ya Lamu ulivyozaliwa kutokana na mapenzi ya Mzee Kenyatta kwa mti wa Mpeketo uliomsitiri.

Kulingana na diwani wa zamani, ambaye pia ni mwanahistoria na mzee wa eneo hilo, Bw Francis Chege, jina Mpeketoni kila linapotajwa huleta kumbukumbu ya yaliyojiri kwa wakati huo, hasa ujio wa Mzee Kenyatta na kubadilishwa jina kwa eneo zima la Mkunguya kuwa Mpeketoni.

“Twafurahia kwamba ujio wa Mzee Jomo Kenyatta eneo letu la Mkunguya miaka ya sabini ulipelekea kuzaliwa kwa jina jipya la eneo hili ambalo ni Mpeketoni. Yaani Mpeketoni ilibandikwa jina hilo kutokana na mti uliomsitiri Mzee Kenyatta wa Mpeketo. Kwa sasa Mpeketoni imekua kihadhi na kuwa eneo muhimu la kutegemewa Lamu, hasa kwa kilimo na maendeleo,” akasema Bw Chege.

Mzee David Muiga wa mjini Mpeketoni anautaja ujio wa Mzee Kenyatta miaka hiyo ya sabini kuwa ulioleta faida tele kwa wenyeji.

Mzee na mwanahistoria wa Mpeketoni, Bw David Muiga. Anasema wakati wa uhai wake, Hayati Mzee Jomo Kenyatta alijibanza kivulini mwa mti wa Mpeketo, hivyo akapenda mandhari kiasi cha kuamuru eneo zima kuitwa Mpeketoni. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Muiga anasema mbali na kumbukumbu aliyoacha ya jina jipya la Mpeketoni, alama nyingine ya kudumu aliyoacha ni ile ya kuligeuza jina la Ziwa kubwa la Mkunguya, ambapo alilibandika jina lake mwenyewe kuwa Ziwa Kenyatta.

Ziwa Kenyatta, ambalo lina ukubwa wa karibu kilomita tano mraba, ndilo ziwa kubwa zaidi na lenye maji yasiyo ya chumvi kote Lamu.

Ziwa hilo linategemewa na zaidi ya wakazi 60,000 wa tarafa ya Mpeketoni na viunga vyake ambao hupata maji ya kunywa na matumizi mengine majumbani.

Ziwa Kenyatta ambalo awali lilikuwa likiitwa Ziwa Mkunguya. Liliitwa Ziwa Kenyatta na Mzee Jomo Kenyatta miaka ya sabini (1970s). PICHA | KALUME KAZUNGU

Wakazi pia hutumia maji ya Ziwa Kenyatta kuendeleza kilimo cha unyunyizaji maji mashambani na pia kunywesha mifugo wao.

“Twafurahia kwamba baada ya kubadilisha jina la eneo la Mkunguya kuwa Mpeketoni kutokana na mti wa Mpeketo aliokaa kujisitiri dhidi ya jua, pia aliamjuru kuanzia siku hiyo kwamba Ziwa Mkunguya liitwe jina lake mwenyewe. Hivyo ndivyo Ziwa Kenyatta linalotambuliwa hadi leo lilibandikwa jina la kiongozi huyo wa taifa.

Lakini je, mti huo wa Mpeketo bado upo Mpeketoni?

Kulingana na mwanahistoria mwingine na mzee wa Mpeketoni, Bw Benson Kariuki, mti mkongwe wa Mpeketo uliozaa Mpeketoni haupo tena.

Mzee wa Mpeketoni, Bw Benson Kariuki akieleza kuwa mti mkongwe wa Mpeketo ulianguka kufuatia maombi yaliyotekelezwa na mhubiri kwa jina Mbugua aliyedai mti huo ulitumiwa vibaya na washirikina na wachawi kulemaza maendeleo Mpeketoni. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Kariuki anaeleza kuwa mnamo miaka ya tisini (1990s), kulikuweko na mwinjilisti mmoja aliyetambuliwa kama Mbugua.

Mwinjilisti huyo anadaiwa kuweka mkutano mkubwa wa injili kwa juma zima mjini Mpeketoni.

Ni wakatio huo ambapo Mwinjilisti Mbugua anadaiwa kutoa njozi iliyomuonyesha jinsi mti fulani mkubwa na mkongwe ulikuwa ukitumiwa vibaya na washirikina, hasa wachawi kutatiza maendeleo ya Mpeketoni.

Juma hilo la injili, Mwinjilisti Mbugua aliwaongoza waumini kuelekea ulipokuwepo mti alioonyeshwa njozini kwa minajili ya kukemea mapepo, washirikina na pia kuagiza mti huo uondolewe kwani ni wenye mikosi.

“Cha kushangaza ni kwamba waumini na wakazi waliohudhuria injili hiyo walielekezwa hadi kwenye mti huo mkongwe wa Mpeketo. Maombi yakafanywa na maagizo kwamba mti uangushwe yakatolewa eti kwa minajili ya kusitisha wachawi na washirikina walioutumia mti huo vibaya. Siku iliyofuatia, watu walipata mshangao mwingine kwani mti huo ulipatikana umenyauka upande mmoja,” akasema Bw Kariuki.

Baada ya majuma kadhaa kupita, mti huo wa Mpeketo ulianguka na hivyo ndivyo ilivyokuwa hatima ya mti huo.

“Mti ulisalia magogo yaliyooza na kuozeana. Leo hii hata hivyo tuko na bahati kwani kuna Mipeketo au miti midogo midogo ya Mpeketo ambayo imemea kando kando mwa Ziwa Kenyatta. Pia tunafanya juhudi kupanda miti ya mipeketo maeneo mbalimbali ya Mpeketoni. Tuko na fahari na mti wa Mpeketo kwani ndio uliotuzalia jina Mpeketoni,” akasema Bw Kariuki.