Habari za Kitaifa

Jinsi mwimbaji maarufu wa Ohangla aliuawa katika makazi ya kifahari

May 11th, 2024 1 min read

STANLEY NGOTHO NA LABAAN SHABAAN

MAKACHERO wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wanachunguza chanzo cha kifo cha msanii wa Ohangla Bi Sheila Odoyo, maarufu Sheila Wegesha, mwenye umri wa miaka 38.

Ripoti ya polisi inaarifu mnenguaji mauno huyo alipatikana amefariki kitandani mwake akilowa damu mnamo Alhamisi Mei 9 mtaani Hill View, Athi River, Kaunti ya Machakos.

“Mwili wake ulikuwa kitandani akiwa na alama kubwa ya kisu shingoni na damu kwenye godoro,” ripoti ilionyesha.

Binti yake, mchanga aliambia polisi kuwa alijua kuhusu kifo hicho Alhamisi adhuhuri alipoenda kumpa chakula cha mchana.

Mume wake anashukiwa na wapelelezi kuwa ana ufahamu kuhusu tukio hilo la kutisha.

Inaripotiwa kuwa aliondoka nyumbani mwake saa saba usiku wa kuamkia Alhamisi akitumia gari lenye nambari ya usajili KDM 798M aina ya Mitsubishi Outlander.

Anashukiwa kwa sababu hakusema lolote kuhusu kifo hicho kinachodhaniwa kilitekelezwa kwa njia ya kikatili.

Maiti inahifadhiwa katika makafani ya hospitali ya Shalom Community polisi wakiendelea kutegua kitendawili cha unyama huo.

Mpelelezi mmoja amefichua kwa Taifa Leo kuwa mumewe ndiye mshukiwa mkuu.

“Kulikuwa na ishara ya mvutano kwenye chumba cha malezi. Tunamshuku mume wake lakini bado hatujapata silaha iliyotumiwa,” alieleza bila kufichua kama mume huyo alitoa ripoti kwa polisi.

Jirani mmoja aliyezungumza na Taifa Leo mnamo Ijumaa alisema kuwa wanandoa hao walikuwa na ugomvi wa kawaida katika uhusiano.

“Kila ndoa ina pandashuka zake. Inasikitisha kuwa hii iliisha vibaya,” alisema kwa ufupi.

Inaripotiwa kuwa marehemu alikuwa na duka la pombe mtaani Umoja ambalo waliendesha pamoja na mumewe.

Bi Odoyo alikuwa maarufu katika maeneo ya burudani yanayopiga nyimbo za Kidholuo za Ohangla jijini Nairobi na viunga vyake.

Msakataji densi huyo ameombolezwa na mashabiki katika mitandao ya kijamii nchini na ughaibuni wakisambaza picha za wachumba hao wakiwa na furaha siku zilizopita.