Makala

Jinsi mzee alivyouawa na gari la mbunge aliyempigia kampeni

March 14th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

MZEE Amos Mwangi, 60, alipompigia kampeni Mary Wamaua kuwa mbunge wa Maragua, hakuna aliyedhania kuwa siku moja angeuawa na gari la mwanasiasa huyo.

Mzee Mbau kutoka kijiji cha Waruri kilichoko karibu na mji wa Kaharati, alikuwa kiungo muhimu katika kampeni za Mbunge wa Maragua Mary wa Maua alipokuwa akisaka awamu ya pili katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Mzee huyo alikuwa akivalia shati-tao la nembo ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) pamoja na picha ya mwanasiasa huyo.

Hatimaye, Bi wa Maua alishinda uchaguzi huo na mzee huyo akawa mmoja wa wafuasi wake waliofurahia tukio hilo kwa dhati.

Lakini mnamo Machi 2, 2024, Mzee Mbau alipigiwa simu na watu wa familia yake wanaoishi katika mji wa Kabati ulioko katika eneobunge jirani la Kandara.

Walimweleza kuwa walikuwa wakihitaji maparachichi ya kula nyumbani kwao.

“Alienda shambani na akavuna takriban maparachichi 50 na akayaweka kwa gunia. Kisha alienda kwa steji ya magari ya kuenda mjini Thika na jijini Nairobi na akapeana mzigo huo kwa gari moja,” asema msemaji wa familia hiyo Bw Samuel Maina.

Mpango ulikuwa kwamba wapokeaji wa mzigo wangewasiliana na dereva wa gari hilo ili wapate maparachichi yao likifika mjini Kabati.

Bw Maina alisema kwamba Mzee Mbau baada ya kuwapasha hao waliokuwa Kabati kwamba tayari alikuwa ametuma mzigo, alitumiwa kwa simu pesa.

Mzee huyo aliamua kuingia kwa baa kujiburudisha.

“Mwendo wa saa kumi jioni Mzee Mbau alitoka kwa baa iliyokuwa karibu na boma lake katika mkondo wa barabara ya kutoka Kamahuha hadi Kaharati,” akaeleza Bw Maina.

Lakini gari la Bi wa Maua lilimgonga akivuka barabara.

Aligongwa kiasi kwamba gari lilimuinua na kupaa angani kwa muda kabla ya kurejea kwa lami kwa kishindo.

Alipata majeraha na damu ikaanza kuvuja.

Walioshuhudia ajali hiyo wakiwemo wahudumu wa bodaboda walifuata gari hilo kwa kuwa dereva walo hakulisimamisha baada ya ajali hiyo.

Kwa mujibu wa Bw Stephen Ndukwa ambaye alishuhudia kisa hicho, wahudumu wa bodaboda hao walifanikiwa kulizuia gari hilo.

“Mheshimiwa hakuwa ndani ya gari hilo, ni dereva tu aliyekuwa nalo,” akasema Bw Ndukwa.

Maafisa wa polisi walifika dakika chache baadaye na wakamwagiza dereva wa mheshimiwa kuliwasilisha gari hilo la ajali hadi katika kituo cha polisi cha Maragua.

Naye Mzee Mbau alikuwa katika hali isiyoeleweka na alipelekwa hadi stesheni hiyo ili idhini itolewe ya kumpeleka katika mochari.

“Lakini ilikadiriwa kwamba kwanza apelekwe katika hospitali ya Maragua ndipo madaktari wathibitishe kwamba Mzee Mbau alikuwa ameaga dunia au la. Pale hospitalini ilibainika hakuwa ameaga dunia,” Bw Maina akasema.

Lakini kwa kuwa majeraha yake yalikuwa mabaya hasa kwa kichwa, alihamishwa hadi katika Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH).

Mzee Mbau ambaye mkewe aliaga dunia mwaka wa 2022 na akiwa baba wa watoto watatu, alikaa katika wadi ya wagonjwa mahututi hadi Machi 6, 2024, alipoaga dunia.

Ripoti ya polisi wa Maragua ilirekodi ajali hiyo kama tukio nambari 25 la Machi 2, 2024.

Ilirejelea tukio hilo kama ajali ya barabarani lakini mnamo Machi 11, 2024 , polisi waliifanyia marekebisho na kuitaja rasmi kama ajali iliyosababisha kifo.

Naye dereva wa gari hilo la mheshimiwa baadaye alifika katika kituo cha polisi cha Sabasaba kilicho karibu na nyumbani kwake mbunge huyo na kurekodi taarifa kwamba alipigwa na washukiwa wawili waliomkabili katika eneo la ajali.

Maafisa hao nao walianza msako ambao uliishia kukamatwa kwa Bw James Ngugi Gatonga na Bw Boniface Kamau mnamo Machi 9 na Machi 10, 2024, mtawalia.

Mnamo Machi 11, 2024, wawili hao waliambia Taifa Leo kwamba waliachiliwa baada ya kulipa Sh4,000 kila mmoja, pesa ambazo haieleweki zilikuwa za nini kwa kuwa hazijarekodiwa kama ni fidia, bondi au hongo.

Kamanda wa Polisi wa Murang’a Mathiu Kainga alisema kwamba madai hayo ya malipo katika kituo hicho cha Sabasaba yanachunguzwa ili kubaini mazingara kamili kuyahusu.

Uchunguzi huo ukiendelea, nao mwili wa Mzee Mbau unazidi kukaa katika mochari ya Kenyatta kutokana na bili ya Sh300,000 kufikia Machi 12, 2024.

Familia ya mwendazake sasa inahoji ilikuwaje vituo viwili vya polisi vilibishania kushughulika na kisa hicho cha ajali?

Kile cha Maragua kilifuata uchunguzi wa ajali nacho kile cha Sabasaba kikifuatana na kuwakamata mashahidi waliokuwa katika eneo la ajali.

Bw Kainga alisema kwamba kisa hicho kitachunguzwa kwa uadilifu na sheria ya kudumisha haki itekelezwe, huku familia ikimtaka kamanda huyo ahakikishe hakutakuwa na ukora katika kuafikia malengo ya kisheria katika kisa hicho.

[email protected]